Kuongezeka mauzo ya bidhaa za Iran nchini Iraq
(last modified 2024-09-12T11:34:14+00:00 )
Sep 12, 2024 11:34 UTC
  • Kuongezeka mauzo ya bidhaa za Iran nchini Iraq

Shirika la Maendeleo ya Biashara la Iran limetangaza kuwepo ongezeko kubwa la mauzo ya Iran nchini Iraq katika miezi ya karibuni.

Shirika hilo limesema katika miezi mitano ya karibuni, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeweza kuuza nchini Iraq bidhaa za thamani ya zaidi ya dola bilioni nne na milioni 500, ambalo ni ongezeko la asilimia 27 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.

Gesi asilia, maji ya chuma, vigae vya ujenzi, aina mbalimbali za chuma, viyoyozi vya maji, viazi, matikiti maji, vifaa vya nyumbani, nyanya na vifaa vya jikoni vya plastiki ni miongoni mwa bidhaa ambazo ziliuzwa kwa wingi nchini Iraqi katika kipindi hicho.

Mabadilishano ya kibiashara na kiuchumi kati ya Iran na Iraq yameongezeka katika miaka ya hivi karibuni, na ni kuhusiana na hilo, ndipo Rais Masoud Pezeshkia wa Iran, akaitembelea Iraq kuanzia jana Jumatano katika safari ya siku tatu huku akiongoza ujumbe wa ngazi za juu wa kibiashara, kiuchumi na kisiasa kwa ajili ya kuimarisha uhusiano na nchi hiyo jirani. Miongoni mwa nchi za Kiarabu za Asia Magharibi, Iraq ina mafungamano makubwa na mengi zaidi ya kiutamaduni na kidini na Iran.

Kuwa na mpaka mrefu zaidi kati ya majirani wa Iran, wenye urefu wa karibu kilomita 1258 wa nchi kavu na kilomita 351 wa majini, mahusiano ya kikabila, kihistoria, lugha, masuala ya kidini usalama wa pamoja na maslahi ya kiuchumi ni nukta muhimu za pamoja katika mahusiano ya nchi hizi jirani na rafiki za Iran na Iraq.

Kuimarishwa mahusiano ya pande mbili ni suala muhimu ambalo limekuwa likifuatiliwa kwa karibu na viongozi wa nchi hizi katika miaka ya karibuni kwa kutilia maanana mafungamano makubwa yaliyopo kati ya mataifa haya, hasa ya kiutamaduni, kisiasa na kidini.

Tags