Sep 13, 2024 02:30 UTC
  • Radiamali ya Iran kwa vikwazo vya nchi za Ulaya dhidi ya Shirika la Ndege la Iran Air

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran ameichukulia kauli ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kuhusiana na kufutwa makubaliano ya pande mbili ya kutoa huduma za anga kwa Iran kuwa ni ugaidi wa kiuchumi wa nchi za Magharibi dhidi ya taifa la Iran.

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imeliwekea vikwazo shirika la ndege la Iran Air ikiwa ni katika kuendeleza vikwazo vya kidhalimu vya nchi hiyo dhidi ya Iran kwa kisingizio cha kutumwa makombora ya Iran nchini Russia ili yatumike katika vita dhidi ya Ukraine.

Kuhusu suala hilo, Nasser Kanani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, amelaani vikali kauli hiyo isiyo ya kawaida kidiplomasia ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kuhusiana na kufutwa makubaliano ya pande mbili ya utoaji huduma za anga kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuwekewa vikwazo shirika la Iran Air kwa kisingizio cha kuingilia mgogoro wa Ukraine.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema: "Tamko la nchi tatu za Ulaya ni kuendeleza siasa za uadui za nchi za Magharibi na vitendo vya ugaidi wa kiuchumi dhidi ya wananchi wa Iran, jambo ambalo litakabiliwa na hatua za kulipiza kisasi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran."

Msemaji huyo wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesisitiza tena msimamo wa wazi na uliotangazwa awali wa Iran kuhusiana na mzozo wa Ukraine na kusema: "Kama ilivyosisitizwa huko nyuma, madai yoyote kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeiuzia Russia makombora ya balistiki hayana msingi wowote na ni uongo mtupu."

Kanani ameongeza kwa kusema: 'Marekani na nchi hizo tatu za Ulaya ndizo chanzo kikuu cha silaha za utawala wa Kizayuni na washirika wake katika mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Palestina huko Ghaza hivyo zinapaswa kuwajibishwa kuhusiana na siasa hizo mbovu na potofu.'

Naye Amir Saeid Iravani, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amekanusha tuhuma zisizo na msingi na za kupotosha zinazotolewa na Marekani, Uingereza na Ufaransa kuhusiana na nafasi ya Tehran katika vita vya Ukraine na kusema: "Marekani na washirika wake hawawezi kuficha ukweli usiopingika kwamba kutumwa silaha za Magharibi na za kiwango cha juu, hasa kutoka Marekani, kumerefusha vita nchini Ukraine na kuwadhuru raia na miundombinu ya kiraia."

Kitendo hiki cha Nchi Tatu za Ulaya kimefanyika sanjari na vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Shirika la Ndege la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (Iran Air) na sambamba na kushadidishwa mashinikizo dhidi ya Tehran kwa lengo la kuweka vikwazo zaidi vya kiuchumi, kibiashara na usafiri kwa Iran hasa kuhusiana na usafiri wa anga kuelekea Ulaya.

Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran

Malengo ya madola ya Ulaya ni kuzuia ndege za abiria na usafiri wa anga za Iran hususan Iran Air zisifikie nchi za Ulaya na hivyo kuzisababishia hasara kubwa za kifedha. Aidha kwa vikwazo hivyo, mashirika  mengine ya ndege yanayoshindana na Iran Air yataweza kuwabeba abiria ambao wamekuwa wakitumia shirika hilo na hivyo kulipokonya soko lake kubwa la abiria.

Aidha, vikwazo ambavyo Iran Air imewekewa na Marekani na Ulaya vitapelekea kukosekana upatikanaji wa vipuri muhimu kwa safari za ndege za abiria. Hivyo kinyume na madai ya Washington, ambayo inadai inawatetea watu wa Iran, vikwazo hivyo vitahatarisha zaidi maisha ya wanaosafiri kwa ndege. Ni wazi kuwa vikwazo hivi ni dhidi ya wananchi wa Iran na ni ishara ya kuongezeka mashinikizo dhidi yao kutoka nchi za Magharibi.

Kuhusiana na hilo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani iliiwekea vikwazo Iran Air siku ya Jumanne ili kuzidisha vikwazo dhidi ya Iran kwa kisingizio kuwa eti Iran inatuma makombora nchini Russia yatumike katika vita dhidi ya Ukraine.

Madai ya Marekani na nchi za Ulaya kuhusu kutumwa makombora ya balistiki kutoka Iran hadi Russia kwa ajili ya matumizi katika vita vya Ukraine yametolewa huku Tehran ikikanusha mara kwa mara madai hayo kuwa hayana msingi wowote.

Kuhusiana na hilo, Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba: "Kwa mara nyingine tena, Marekani na Ulaya zimechukua hatua kwa msingi wa taarifa zisizo sahihi na mantiki yenye dosari. Iran haijaipatia Russia makombora ya balistiki. Wenye uraibu wa vikwazo wanapaswa kujiuliza: Je, Iran inawezaje kutengeneza silaha za kisasa na kuziuza kama mnavyodai? Vikwazo sio suluhisho, bali ni sehemu ya tatizo."

Tags