Tehran, Beirut zajadili jinai mpya ya kigaidi ya Israel huko Lebanon
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi amelaani vikali hujuma mpya ya kigaidi ya utawala wa Kizayuni iliyowalenga raia wasio na hatia nchini Lebanon.
Katika mazungumzo kwa njia ya simu na mwenzake wa Lebanon, Abdullah Bouhabib, Waziri wa Mashauri wa Kigeni wa Iran huku akitoa salamu zake za rambirambi na kueleza mshikamano wake na serikali, taifa, na familia za mashahidi na majeruhi wa tukio hilo la jana nchini Lebanon, ameeleza kuwa Iran iko tayari kutoa msaada wowote kwa ajili ya matibabu ya majeruhi wa shambulio hilo au kuletwa Tehran kutibiwa.
Vile vile ameashiria kujeruhiwa kwa balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mojtaba Amani katika shambulio hilo la kigaidi, na huku akiishukuru serikali ya Lebanon kwa hatua za haraka za matibabu, alielezwa kuhusu hali ya hivi punde ya utaratibu wa matibabu ya mwanadiplomasia huyo wa Iran.
Wizara ya Afya ya Lebanon imesema watu wasiopungua tisa wameuawa na wengine 2,800 wamejeruhiwa katika miripuko ya vifaa vya mawasiliano (pagers) ambayo iliripotiwa kwa mara ya kwanza katika viunga vya kusini mwa Beirut hapo jana.
Miongoni mwa waliouawa shahidi katika jinai hiyo mpya ya Wazayuni ni binti wa miaka 9 na mtoto wa mbunge mwenye mfungamano na Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon.
Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa, miripuko hiyo yumkini ilisababishwa na shambulio la mtandao la kuelekezwa kutoka mbali, lililoratibiwa na utawala wa Israel huku kukiwa na taharuki na mvutano mkubwa baina ya pande mbili.
Hizbullah imelaani shambulio hilo, ikilitaja kuwa ni kitendo cha uadui, na kusisitiza utayarifu wake usio na kifani wa kuilinda Lebanon na kuzima njama na ugaidi wa Israel.