Iravani: Shambulio la Iran la makombora ni jibu kwa ugaidi wa Israel
(last modified Thu, 03 Oct 2024 12:49:27 GMT )
Oct 03, 2024 12:49 UTC
  • Iravani: Shambulio la Iran la makombora ni jibu kwa ugaidi wa Israel

Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa shambulio la makombora ya balistiki la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel la juzi Jumanne lilikuwa jibu la lazima kwa vitendo vya kigaidi vya utawala huo ghasibu katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.

Akizungumza katika kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lenye wanachama 15 jana Jumatano, Amir Saeid Iravani alisema, katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, "utawala wa kibaguzi na ghasibu wa Israel umeendeleza ukatili wake katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu bila kuadhibiwa."

Ameongeza kuwa, "Na sasa, utawala huu umeendeleza vita vyake vya kikatili kwa kuvamia  Lebanon na kulenga watu wasio na hatia mchana na usiku."

Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, Israel ilimuua mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, Ismail Haniya katika mji mkuu wa Iran wa Tehran, na kiongozi wa Hizbullah Sayyid Hassan Nasrallah, na kamanda wa IRGC Abbas Nilforoushan, mshauri wa kijeshi wa Iran nchini Lebanon, katika mji mkuu wa Lebanon wa Beirut.

Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema Israel inalisukuma eneo la Asia Magharibi katika ukingo wa janga kubwa ambalo halijawahi kutokea. Amesema: "Israel haina nia ya kutafuta amani au kusitisha mapigano na cha kusikitisha ni kwamba, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limesalia katika hali ya kupooza kutokana na Marekani kuzuia uamuzi wowote unaofaa wa chombo hiki."