Oct 04, 2024 07:12 UTC
  • Iran yakosoa 'hujuma' ya Israel dhidi ya Katibu Mkuu wa UN

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekosoa vikali hatua ya karibuni ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres.

Esmaeil Baghaei, Msemaji mpya wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa X leo Ijumaa kuwa, hatua ya Wazayuni dhidi ya Guterres ni hujuma na utumiaji wa mabavu unaolenga kumshinikiza Katibu Mkuu huyo wa UN anyamazie kimya jinai za Wazayuni.

Baghaei amesema Israel ni utawala ambao balozi wake wa zamani alichana Hati ya Umoja wa Mataifa machoni pa ulimwengu, na ndio utawala ule ule ambao Waziri Mkuu wake, Benjamin Netanyahu alitumia mkutano wa karibuni wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) kuwatishia walimwengu kuwa atasababisha vifo na uharibifu zaidi duniani. 

Matamshi ya Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran yanakuja baada ya utawala wa Kizayuni wa Israel kumtaja Guterres kuwa ni mtu asiyetakikana eti kwa sababu ya kunyamazia kimya operesheni ya makombora ya Iran ya kulipiza kisasi dhidi ya Israel, na kumpiga marufuku kuingia katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel).

Esmaeil Baghaei, Msemaji mpya wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran

Uamuzi huo wa Israel umepingwa vikali na shakhsia wengi duniani akiwemo Josep Borrell, Mkuu wa Siasa za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, ambao wameutaja kuwa ni kinyume na juhudi za kuimarisha amani katika eneo la Magharibi mwa Asia.

Msemaji mpya wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kukomesha jinai za utawala wa Kizayuni bila kupoteza muda zaidi.

 

Tags