Umuhimu wa kushiriki rasmi Iran katika mkutano wa BRICS
(last modified Wed, 23 Oct 2024 13:07:08 GMT )
Oct 23, 2024 13:07 UTC
  • Umuhimu wa kushiriki rasmi  Iran katika mkutano wa BRICS

Siku ya Jumanne, kabla ya kuondoka kwake nchini kwenda Russia kwa ajili ya kushiriki katika mkutano wa BRICS katika mji wa Kazan, Rais Masoud Pezeshkian wa Iran alisema BRICS ni njia ya kujiimarisha na pia kuondokana na siasa za upande mmoja za Marekani katika mfumo wa dunia.

Jana Jumanne, ikiwa ni safari yake ya tano nje ya nchi na kwa mwaliko wa Rais Vladimir Putin wa Russia kwa lengo la kushiriki katika mkutano wa 16 wa viongozi wa BRICS, Daktari Masoud Pezeshkian aliondoka nchini kuelekea mji wa Kazan kwa ajili ya kushiriki mkutano huo wa kilele wa kundi la BRICS unaofanyika kuanzia tarehe 22 hadi 24 za mwezi huu wa Oktoba. Huu ni uwepo wa kwanza rasmi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mkutano huo kama mwanachama rasmi, ambapo ilikubaliwa kuwa mwanachama kamili katika jumuiya hiyo mnamo Januari mwaka huu.

Kundi la BRICS, au nchi zinazoinukia kiuchumi, awali liliundwa na Russia, China, India na Brazil, na kisha Afrika Kusini ikajiunga nalo. Mwanzoni mwa mwaka huu nchi za Iran, Saudi Arabia, UAE, Misri na Ethiopia pia ziliongezwa kwenye kundi hilo.

Kundi la BRICS ni muhimu sana kisiasa na kiuchumi kwa wanachama na vile vile nchi zisizo wanachama, haswa madola ya Magharibi. Kisiasa, umuhimu wa BRICS ni kwamba inauelekeza mfumo wa ulimwengu kwenye muundo wa pande kadhaa kimataifa tofauti na ulivyo mfumo wa upande mmoja wa Marekani. Kwa kuzingatia kuwa nchi kama vile China, India na Russia ambayo ni mataifa yenye nguvu kubwa duniani na pia nchi kama vile Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Saudi Arabia na Brazil ni mataifa yenye nguvu za kieneo ni wanachama wa kundi hili, ni wazi kuwa ushirikiano wa pande kadhaa unatekelezwa kivitendo.

Rais Masoud Pezeshkian wa Iran awasili katika mji wa Kazan Russia, kushiriki mkutano wa 16 wa wakuu wa Jumuiya ya Kiuchumi ya BRICS

Kuhusiana na suala hilo, kikao cha wakuu wa nchi za BRICS kinafanyika huko mjini Kazan, nchini Russia chini ya kaulimbiu ya "Kuimarisha Ushirikiano wa Kimataifa" kwa kuhudhuriwa na wanachama wa BRICS-Plus na kingine kinafanyika katika mji huo huo kwa ushiriki wa takriban nchi na mashirika ya kimataifa 30 chini ya kaulimbiu ya  "BRICS  na Kusini mwa Dunia." Katika mkutano na waandishi wa habari kabla ya kuondoka kwake nchini kuelekea Russia,  Rais Masoud Pezeshkian alisema kuwa BRICS ni jumuiya ambayo iliundwa kwa ajili ya kuanzisha umoja na mshikamano kati ya nchi wanachama na wakati huo huo kudhibiti nguvu isiyo na mpinzani ya Marekani na madola ya Magharibi. Kundi hili bila shaka linaweza kudhibiti siasa za upande mmoja za Marekani.

Katika mtazamo wa kiuchumi pia, kundi la BRICS lina uwezo mkubwa wa kiuchumi ambapo linamiliki takriban asilimia 30 ya uchumi wa dunia, na suala hili linaweza kuongeza ushirikiano wa kiuchumi na maingiliano kati ya nchi wanachama, na wakati huo huo kukabiliana na vitisho vya Marekani ambavyo vinahatarisha maslahi ya baadhi ya nchi wanachama.

Kumiliki asilimia 30 ya uchumi wa dunia pamoja na nusu ya idadi ya watu duniani, pembeni ya tishio la pamoja la vikwazo vya kidhalimu kutoka Marekani, kunaweza kuweka msingi mzuri wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi wanachama wa BRICS na wakati huo huo kutumika fursa mahsusi zilizopo kwa ajili ya kuvuka tishio hilo la vikwazo vya kidhalimu.

Kuanzishwa kwa mfumo wa malipo wa "BRICS Pay" kunaweza kupunguza utegemezi wa nchi wanachama wa BRICS kwenye dola ya Marekani na mfumo wa kifedha wa Magharibi, na hivyo kuwezesha miamala ya kimataifa bila kuishirikisha Marekani.

Mfumo huu, unaoazimia kuchukua nafasi ya SWIFT, unaweza kuzisaida nchi zilizo chini ya vikwazo vya Marekani kufanya miamala yao ya kifedha bila kutegemea mfumo wa kifedha wa madola ya Magharibi.