Salami: Muqawama utatoa jibu kali dhidi ya kambi ovu
(last modified Sun, 03 Nov 2024 12:02:05 GMT )
Nov 03, 2024 12:02 UTC
  • Salami: Muqawama utatoa jibu kali dhidi ya kambi ovu

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) amezionya vikali Marekani na Israel kwamba, uvamizi na kitendo chochote cha kichokozi kitakabiliwa na jibu zito la 'kuvunja meno' la makundi ya Muqawama ya eneo la Asia Magharibi.

Meja Jenerali Hossein Salami ameyasema hayo leo Jumapili katika hotuba yake aliyoitoa kwa mnasaba wa kuadhimisha Siku ya Kitaifa ya Kupambana na Uistikbari wa Dunia, ambayo pia inajulikana kama Siku ya Kitaifa ya Wanafunzi.

Siku hii inaadhimisha kutekwa pango la ujasusi (Ubalozi wa Marekani) mwaka 1979 na wanafunzi wa vyuo vikuu vya Iran katika mji mkuu Tehran. Jenerali Salami ameipongeza siku hii ya kihistoria "isiyofutika" katika kufichua hali halisi ya Marekani na uovu wake dhidi ya mataifa yanayopenda uhuru na haki duniani.

Salami amesema ukatili wa Israel, unaofanywa chini ya amri na uungaji mkono wa pande zote wa utawala wa Washington, dhidi ya eneo la kimkakati la Asia Magharibi, dhidi ya watu wasio na hatia katika Ukanda wa Gaza na Lebanon, unaonekana 'halali' kutokana na kupotea kwa haki za binadamu za Marekani.

Wairani katika maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Uistikbari

Jenerali Salami amesema, "Tunamuonya adui nambari moja wa taifa la Iran na mbwa kichaa wa utawala huo wa kigaidi na jinai kwamba, Muqawama wa Kiislamu katika eneo hili, kwa neema ya Allah na kwa msaada wa ujasiri wa wapambanaji mashupavu na wapiganaji waaminifu wenye 'mkono wa juu' katika uwanja wa sasa wa kijeshi, utatoa jibu la kuvunja meno kwa mrengo wa uovu."

Kamanda Mkuu wa Jeshi la SEPAH la Iran ameongeza kuwa, "Katika njia hii, mrengo wa Muqawama na Iran ya Kiislamu zitajizatiti kwa kila linalohitajika ili kukabiliana na kuwashinda adui kwa ushindi, bila woga wowote wa vitisho na kelele za majambazi wanaotawala Washington na Tel Aviv.”