Kamanda Fadavi: Vita vya Ghaza vimefedehesha uongo wa miaka 76 wa mabeberu
(last modified Mon, 04 Nov 2024 02:41:38 GMT )
Nov 04, 2024 02:41 UTC
  • Kamanda Fadavi: Vita vya Ghaza vimefedehesha uongo wa miaka 76 wa mabeberu

Kaimu Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH amesema kuwa, Marekani ndiye kiranja wa kambi ya batili na kwamba, moja ya sifa za kipekee za vita vya Ghaza ni kuwa walimwengu wamezinduka na wameweza kuelewa kwamba wamekuwa wakidanganywa na mabeberu kwa muda wa miaka 76 kuhusu Palestina na utawala wa Kizayuni.

Hayo yameripotiwa na shirika la habari la FARS ambalo limemnukuu Kamanda Ali Fadavi akisema hayo jana kwa mnasaba wa Aban 13 - siku ambayo hapa Iran inajulikana kwa jina la Siku ya Taifa ya Kupambana na Uistikbari - na kuongeza kuwa, tangu wanachuo wa Iran walipouteka ubalozi wa Marekani mjini Tehran miaka 45 iliyopita mpaka leo hii, Marekani imeshindwa kufanya jeuri yoyote ile nchini Iran.

Maandamano ya Aban 13 mjini Tehran

 

Amesema kuwa tangu wakati huo hadi hivi sasa, uadui na ukhabithi wa Marekani haujapungua hata chembe na hata kwa sekunde moja lakini kwa baraka za vita vya kujihami kutakatifu na jitihada na mipango mizuri, Mwenyezi Mungu amejaalia Marekani isithubutu kulenga hata risasi moja dhidi yetu. Hii ni kwa sababu ahadi ya Allah muda wote ni kuwanusuru wanaoinusuru dini yake. Ni ahadi ya Allah ambayo muda wote hutimia ya kwamba Hizbullah, chama cha Allah ndicho kinachoshinda mbele ya chama cha shetani. Ni kwa sababu hiyo ndio maana Marekani imeamua kukimbilia kwenye vita vingine kama vya kiuchumi dhidi yetu baada ya kuona nguvu zetu za kijeshi.

Kaimu Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH amesema pia kuwa, ni wajibu wetu kujiimarisha na kuwa na nguvu katika pande zote ikiwa ni pamoja na kwenye masomo ya vyuo vikuu ili kwa njia hiyo tuweze kumkatisha tamaa adui kikamilifu, katika nyuga zote.