Mkuu wa IRGC: Hizbullah imenusurika kimiujiza
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema licha ya hasara na matukio ya kusikitisha, harakati ya Hizbullah ya Lebanon imejengwa upya kimiujiza.
Meja Jenerali Hossein Salami aliyasema hayo Jumatano ikiwa ni zaidi ya mwezi mmoja baada ya utawala wa Israel kumuua shahidi Sayyed Hassan Nasrallah katika shambulio la kigaidi lililofanyika kusini mwa Beirut. Kabla na baada ya tukio hilo utawala ghasibu wa Israel umewaua kigaidi makamanda wengi wa ngazi za juu wa harakati hiyo ya mapambano ya Kiislamu.
Jenerali Salami amesema kwamba: "Utawala wa Kizayuni ulifikiri kwamba kwa kuwaua viongozi na makamanda wa Hizbullah, ungeweza kusitisha uwezo wa kivita wa kundi hili la muqawama."
Amebaini kuwa "Sasa, Hizbullah inasimama kishujaa na kwa ujasiri uwanjani dhidi ya utawala wa Kizayuni, huku mlingno wa nguvu ukiwa unabadilika kila siku kwa maslahi ya Hizbullah."
Jenerali Salami kisha amegusia Operesheni ya Ahadi ya Kweli I ya tarehe 13 Aprili na ya Ahadi ya Kweli II mnamo Oktoba 1, ambayo ilishuhudia Jamhuri ya Kiislamu ikirusha mamia ya makombora ya balistiki dhidi ya ngome za kijeshi na kijasusi za Israel katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Operesheni hizo zilitekelezwa na Iran ili kulipiza kisasi kwa vitendo vya uchokozi wa kutisha vya utawala huo ghasibu. Katika kuendeleza uchokozi wake mapema Oktoba 26, ndege za kivita za Israel zilitumia kituo cha wanajeshi wa Marekani nchini Iraq kurusha makombora ya masafa marefu dhidi ya vituo vya kijeshi katika mikoa ya Tehran, Khuzestan na Ilam nchini Iran. Hujuma hiyo liliwaua maafisa wanne wa Jeshi la Iran na raia mmoja. Mkuu huyo wa IRGC amesema Israel inakosea iwapo inadhani kuwa Iran haitatoa jibu kwa mashambulizi hayo.