Ghalibaf : Kuuawa shahidi Sayyid Nasrullah kumeonyesha ubatili wa kufanya mapatano na Israel
(last modified Sat, 09 Nov 2024 12:25:09 GMT )
Nov 09, 2024 12:25 UTC
  • Ghalibaf : Kuuawa shahidi Sayyid Nasrullah kumeonyesha ubatili wa kufanya mapatano na Israel

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran), Mohammad Baqer Ghalibaf amesema kuuawa shahidi aliyekuwa Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon, Sayyid Hassan Nasrullah kulifichua namna utawala wa Kizayuni usivyoheshimu mapatano ya aina yoyote.

Akihutubia Kongamano la Kimataifa la Kuwaenzi Viongozi wa Muqawama lililopewa jina la 'Fikra ya Nasrullah' hapa mjini Tehran leo Jumamosi, Ghalibaf amesema, "Zimepita siku 40 tangu tuanze kuomboleza kumpoteza ndugu yetu mpendwa, na nembo azizi ya Muqawama. Lazima tumuenzi shakhsia huyo mkubwa asiye na kifani."

Kongamano hilo limefanyika sambamba na maadhimisho ya Arubaini ya kuuawa shahidi Sayyid Nasrullah katika shambulizi la kigaidi na la kinyama la Wazayuni maghasibu huko Beirut.

Spika Ghalibaf ameeleza kuwa, umma wa Kiislamu unapasa kugeuza kuuawa shahidi Nasrullah kuwa nyenzo ya kudumu kwa ajili ya kuendeleza urithi wake na kutimiza mikakati na maazimio ambayo alisabilia maisha yake.

Amegusia pia uungaji mkono usiotetereka wa Nasrullah kwa wapambanaji wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas yenye makao yake Gaza, tangu kuanza kwa Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa mnamo Oktoba 7, 2023.

Spika wa Bunge la Iran amemnukuu Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei akisema: "Kila kipigo dhidi ya utawala wa Kizayuni, na mtu au kikundi chochote, si kwa maslahi ya eneo (la Asia Magharibi) pekee, bali kwa wanadamu wote."

Mkutano huo wa 'Maktaba ya Nasullah' uliofanyika katika Ukumbi Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC, umehudhuriwa na wanazuoni kutoka nchi 13, zikiwemo Lebanon, Iraq, Bahrain, Misri, Kuwait, Uturuki, India, Malaysia, Algeria na Tunisia.