Shahidi Nasrullah, nembo azizi ya muqawama na mapambano dhidi ya dhulma
Kongamano la Kimataifa la Fikra za Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa zamani wa Hizbullah ya Lebanon, limefanyika mjini Tehran kwa lengo la kuchunguza na kutambua mielekeo mbalimbali ya kifikra na kimaarifa ya shahidi huyo pamoja na nafasi yake ya kisiasa katika kukabiliana na kiburi cha Wazayuni, ambapo wataalamu na wanafikra kutoka nchi 13 wameshiriki.
Kongamano hilo ambalo limefanyika sambamba na maadhimisho ya Arubaini ya kuuawa shahidi Sayyid Nasrullah katika shambulizi la kigaidi na la Wazayuni maghasibu huko Beirut, mji mkuu wa Lebanon, limemtaja shahidi huyo mwanamapambano kuwa mwanasiasa mwenye busara, makini na mkamilifu katika masuala ya kitaifa, kikanda na kimataifa katika medani ya vita.
Mohammad Baqer Ghalibaf, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran), amesisitiza katika kongamano hilo kuwa Shahidi Nasrullah pamoja na Mujahidina wa Hamas, waliamini kwamba hakuna vita vilivyo halali kama vita dhidi ya Wazayuni.
Akizungumza katika kongamano hilo la Kimataifa la Kuwaenzi Viongozi wa Muqawama, Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni pia amesema kwamba, Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah ni shakhsia ambaye alikuwa nembo ya muqawama, ujasiri na kusimama kidete dhidi ya dhulma na uvamizi wa utawala katili wa Israel sio tu kwa watu wa Lebanon, bali kwa ulimwengu mzima wa Kiislamu na mataifa yanayopigania uhuru na ukombozi.
Sayyed Abbas Salehi, Waziri wa Utamaduni na Miongozo ya Kiislamu wa Iran pia amesema katika kongamano hilo kwamba Shahidi Hassan Nasrullah alikuwa shakhsia muhimu wa Kiislamu kimataifa, na kwamba ni nadra sana kwa mtu kuwa na mvuto na sifa zote hizo kitaifa, kieneo na kimataifa.
Nasrullah aliuawa shahidi tarehe 27 Septemba kufuatia kitendo cha kigaidi cha utawala wa Kizayuni huko kusini mwa mji mkuu wa Lebanon, Beirut. Alikuwa katibu mkuu wa tatu wa Hizbullah ya Lebanon na mmoja wa waanzilishi wake. Hizbullah ilipata nguvvu kubwa ya kikanda wakati wa ukatibu mkuu wake (1992-2024). Kukombolewa eneo la kusini mwa Lebanon kutoka kwenye makucha ya utawala wa Kizayuni, kuachiliwa huru mateka wa Lebanon na kurejeshwa miili ya mashahidi wa muqawama kutoka mikononi mwa utawala katili wa Israel pamoja na ushindi wa vita vya siku 33, yote hayo yalifanyika katika kipindi cha uongozi wake.
Sayyid Hassan Nasrullah anajulikana kuwa kiongozi mahiri na shupavu kwa sababu, akiwa kiongozi wa muqawama nchini Lebanon, alikuwa na ujasiri wa kuleta mabadiliko na kuendeleza malengo ya Hizbullah, hususan katika suala zima la ukombozi wa Palestina na kulinda mipaka ya Lebanon. Hakuwa tu kiongozi wa kijeshi, bali pia alikuwa mtu wa kuwapa moyo vijana wengi na vizazi vipya waliokuwa wakitafuta njia ya kukabiliana na ukandamizaji na uchokozi wa maadui.
Wakati huo huo utawala wa Israel kufuatia kushindwa kwake katika vita vya Gaza ambavyo vimepelekea makumi ya maelfu ya Wapalestina kuuawa shahidi, uliamua kumuua kinyama Sayyid Hassan Nasrullah, ili kubadilisha hali ya mambo kwa maslahi yake na kufanya Hizbullah ishindwe kufikia malengo yake huko Lebanon na katika kuunga mkono kadhia ya Palestina. Lakini badala yake kuuawa shahidi Nasrullah sio tu kwamba kumeufanya mhimili wa muqawama kuwa na dhamira ya dhati na azma thabiti ya kufikia malengo yake, ambayo ni pamoja na kuirejesha Palestina kwa wamiliki wake halisi, bali pia kumeimarisha mshikamano na azma ya makundi ya muqawama ya kupambana na maghasibu wa Quds Tukufu. Ni kama alivyosisitiza Sheikh Naim Qasim, Katibu Mkuu mpya wa Hizbullah nchini Lebanon katika siku ya kumbukumbu ya siku ya 40 ya kuuawa shahidi Sayyid Hassan Nasrullah kwa kusema: "Muqawama ungali una nguvu katika azma na mwendelezo wake. Ingawa kuna tofauti kubwa katika vifaa na zana za kijeshi kati yetu na adui, lakini thamani kubwa ya damu ya mashahidi ni gharama tunayopasa kulipa kwa ajili ya kupata ushindi na kujisalimisha ni jambo lisilokubalika kabisa. Sisi hatuwezi kushindwa kwa sababu ardhi ni yetu na haki iko upande wetu."
Kwa hakika, kuuawa shahidi Sayyid Hassan Nasrullah akiwa kama ishara ya kusimama imara na kujitolea mhanga kumezidi kuwa msukumo kwa nguvu za muqawama na chanzo cha umoja na mshikamano baina ya makundi ya muqawama na nchi zinazouunga mkono.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, ameitaja Hizbullah kuwa kumbukumbu ya kudumu ya Shahidi Nasrullah na kusema: "Hizbullah, kutokana na ushujaa, busara, subira na imani ya ajabu ya Sayyid wa Muqawama, imepata ukuaji wa ajabu kwa namna ambayo adui aliyejizatiti kwa kila aina ya silaha za kimaada na za kipropaganda hajaweza na kwa neema ya Mwenyezi Mungu, hataweza kamwe kulishinda dhihirisho hili la ajabu.
Bila shaka, mhimili wa muqawama umeazimia kufuata na kuendeleza kwa uthabiti na ujasiri njia uliyoonyeshwa na Shahidi Nasrullah hadi ukombozi wa Palestina utakapopatikana. Kama ilivyosisitizwa katika kongamano la karibuni la mjini Tehran; Jina na urithi wa Sayyid Hassan Nasrullah utaendelea kuwa hai na njia aliyoianzisha itaendelea kwa azma na mapambano zaidi ya vizazi vipya.