Azma ya Iran na Saudi Arabia ya kuimarisha uhusiano baina yao
Viongozi wa ngazi ya juu wa majeshi ya Iran na Saudi Arabia wamejadili njia za kuboresha diplomasia ya ulinzi kati ya nchi mbili huku utawala wa Kizayuni wa Israel ukiendelea kuzidisha mivutano na wasiwasi katika eneo la Magharibi mwa Asia.
Fayyadh bin Hamid al Ruwaili mkuu wa vikosi vya ulinzi wa Saudi Arabia juzi Jumapili aliwasili hapa mjini Tehran kwa lengo la kukutana na kufanya mazungumzo na maafisa wa ngazi ya juu wa kijeshi wa Iran.
Katika mazungumzo hayo, Meja Jenerali Mohammad Bagheri Mkuu wa Majeshi ya Iran na al Ruwaili walibadilishana mawazo kuhusu namna ya kuboresha ushirikiano wa kiulinzi kati ya pande mbili.
Bagheri ametilia mkazo umuhimu wa kuboresha ushirikiano wa pande mbili katika nyanja za ulinzi na kubadilishana uzoefu wa kitaaluma na michezo.
Bagheri pia ameipongeza Saudi Arabia kwa kuandaa mkutano wa aina yake wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) ambao amesema unaweza kuimarisha maelewano kati ya mataifa ya Kiislamu. Mkuu wa Majeshi ya Iran pia amemwalika Waziri wa Ulinzi wa Saudi Arabia kufanya ziara hapa nchini.
Fayyadh bin Hamid al Ruwaili Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Saudi Arabia amesema katika mazungumzo hayo kuwa, makubaliano ya Beijing ni fursa ya kimkakati kwa Tehran na Riyadh kuimarisha ushirikiano wa pande mbili.
Amesema, Iran na Saudi Arabia zina nafasi kubwa katika kuhimiza umoja na mshikamano kati ya Waislamu na nchi za kanda hii na amesisitiza umuhimu wa kuimarishwa ushirikiano wa kisiasa na kiulinzi kati ya pande mbili.
Uhusiano kati ya Iran na Saudi Arabia uliingia katika kipindi kipya tangu Machi mwaka jana (2023) baada ya makubaliano ya Beijing China, na nchi hizo mbili zimechukua hatua ya kuendeleza uhusiano wa pande mbili baada ya miaka saba ya mvutano.
Moja ya ishara za azma ya Tehran na Riyadh za kustawisha uhusiano wa pande mbili ni safari za kidiplomasia zinazofanywa baina ya pande hizo mbili, ambapo maafisa wa kisiasa wa Iran na Saudi Arabia wamekuwa wakifanya safari hadi Riyadh na Tehran na kukutana na kujadili matukio ya kieneo na uhusiano wa pande mbili.
Katika kipindi cha chini ya miezi miwili iliyopita, safari kadhaa za kidiplomasia zimefanywa na maafisa wa nchi hizo mbili. Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Sayyid Abbas Araghchi alitembelea Riyadh, mji mkuu wa Saudi Arabia, mwezi mmoja uliopita yaani mwanzoni mwa mwezi wa Oktoba, ambapo sambamba na kukutana na kufanya mazungumzo na Faisal bin Farhan al-Saud Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa nchi hiyo, pia alikutana na Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia Mohammed bin Salman.
Kazem Gharibabadi, Katibu Mkuu wa Tume ya Haki za Binadamu ya Idara ya Mahakama ya Iran na Naibu wa Kisheria na Kimataifa wa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran pia alitembelea Saudi Arabia siku chache zilizopita. Kadhalika Mohammad-Reza Aref, Makamu wa Kwanza wa rais na Seyyed Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, siku ya Jumapili tarehe 10 Novemba walielekea Saudi Arabia.
Katika mlolongo huo pia, siku hiyo hiyo Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian alifanya mazungumzo ya simu na Mwanamfalme wa Saudia, Mohammed bin Salman na kueleza hamu na shauku ya Iran ya kupanuliwa zaidi ushirikiano baina ya Riyadh na Tehran. Kwa upande wake, Mwanamfalme wa Saudia alipongeza mabadiliko ya kihistoria katika uhusiano wa Tehran na Riyadh na kueleza matumaini yake kuwa, uhusiano wa pande zote mbili utafikia viwango vya juu katika nyanja zote.
Nukta muhimu ni kwamba, ziara ya mkuu wa majeshi ya Saudi Arabia mjini Tehran inaweza kuwa na umuhimu maradufu. Hii ni kwa sababu tofauti na mikutano ya kisiasa na kidiplomasia, ziara za maafisa wa kijeshi wa nchi hizo mbili hufanyika kwa nadra sana.
Hii inaonesha kuwa, uhusiano kati ya Iran na Saudi Arabia uko kwenye mkondo sahihi na haujaathiriwa na matukio ya nchi nyingine au ukosefu wa usalama uliopo katika eneo la Asia Magharibi.
Safari na mazungumzo ya Mkuu wa majeshi ya Saudia na maafisa wa kijeshi wa Iran yamefanyika siku chache baada ya Donald Trump kushinda kinyang’anyiro cha kuingia Ikulu ya White House kwa mara nyingine tena kwa baada ya kushinda uchaguzi wa rais wa Marekani. Wakati wa muhula wa kwanza wa urais wa Trump, Tehran na Riyadh zilikuwa na uhusiano uliokuwa na mvutano.
Licha ya kuwa, vyombo vya habari havijatangaza maelezo ya kina kuhusu mkutano kati ya Wakuu wa Majeshi ya Iran na Saudi Arabia, lakini baadhi ya duru zimeripoti kuwa, Meja Jenerali Mohammad Bagheri Mkuu wa Majeshi ya Iran alisema katika mazungumzo hayo kwamba: Iran ina inapenda kuona Jeshi la Wanamaji la Saudi linashiriki au linakuwa mwangalizi katika mazoezi ya wanamaji wa Iran mwaka ujao katika maji ya Ghuba ya Uajemi.
Nukta ya mwisho ni kwamba, vikao vya kidiplomasia na vilevile matamshi ya viongozi wa Saudia na Iran yanaonesha kuwa, nchi hizo mbili zimezingatia na kulifanya suala la kukuza uhusiano wa pande mbili kuwa ndio kipaumbele katika agenda zao.
Ni wazi kwamba, kuimarishwa uhusiano kati ya Iran na Saudi Arabia yakiwa mataifa mawili muhimu katika matukio ya kieneo kunaweza kuwa muhimu sana hasa kwa ajili ya kutatua migogoro ya sasa ya Asia Magharibi, likiwemo suala la Palestina.