Iran mhanga mkubwa zaidi wa silaha za kemikali
Katika mkutano wa 29 wa mwaka wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Silaha za Kemikali (CWC) huko The Hague, nchi za Magharibi zimenyamazia kimya orodha ya jinai zao za kutumia silaha za kemikali.
Hii ni katika hali ambayo, nchi za Magharibi zinaituhumu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo ndiyo mhanga mkubwa zaidi wa silaha za kemikali kwamba, inataka kuzalisha silaha za maangamizi ya umati.
Kazem Gharibabadi, naibu wa kisheria na kimataifa wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika hotuba yake katika mkutano huo amesisitiza kuwa, Iran ndiyo mhanga mkubwa zaidi wa silaha za kemikali katika zama hizi na amelaani vikali jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watu wa Palestina na Lebanon. Alisema: Utawala huu, kwa uungaji mkono usio na masharti wa baadhi ya nchi za Magharibi, hasa Marekani, unaendelea na jinai zake na una kinga katika hilo.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran katika masuala ya kisheria ameashiria uungaji mkono wa nchi za Magharibi kwa utawala wa Saddam katika vita vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema: Ujerumani na Marekani zikiwa wadhamini wakuu wa mada za kemikali kwa utawala wa Baath wa Iraq ni washirika wa jinai za kemikali dhidi ya watu wa Iran.
Nchi hizi zinapaswa kuwajibishwa kwa vitendo vyao haramu katika ngazi ya kimataifa na kuwalipa fidia wahanga wa silaha za kemikali za Iran.
Marekani ilishambulia Iraq mwaka 2003 kwa kisingizio cha kuangamiza silaha za kemikali. Hii ni pamoja na ukweli kwamba, Marekani na Ujerumani ziliupa utawala wa Saddam silaha za kemikali. Dikteta huyo wa Iraq alitumia silaha hizi kwa kiwango kikubwa dhidi ya Iran na watu wa Iraq.
Wengi wa waliojeruhiwa kwa kemikali walipelekwa katika hospitali za Ulaya ikiwemo Ujerumani, lakini serikali hizo hizo bado zinatumia undumakuwili kuzuia uharibifu wa silaha za kemikali na hivi sasa zinaunga mkono kwa kiasi kikubwa utawala wa Kizayuni katika matumizi ya silaha za kemikali.
Kazem Gharibabadi amelaani kitendo cha utawala ghasibu wa Israel cha kutumia silaha za kemikali na vitu vingine hatari ikiwemo fosforasi nyeupe na urani iliyodhoofishwa dhidi ya watu wasio na ulinzi wa Palestina na Lebanon na kumtaka Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kuzuia Silaha za Kemikali (OPCW) kufanya uchunguzi wa kina katika suala hili na kuchukua hatua zinazohitajika kuwalinda waathirika.
Wazayuni hawajaacha kufanya jinai yoyote huko Gaza na Lebanon. Moja ya uhalifu huu ni matumizi ya mabomu yenye fosforasi nyeupe na urani iliyodhoofishwa. Matumizi ya mabomu haya yanamaanisha mauaji ya umati ya wakazi wa eneo fulani na kuchafua eneo hilo.
Wanaodai kuangamizwa silaha za maangamizi hawako tayari kutimiza wajibu wao wa kuharibu silaha za kemikali licha ya kuwa ni wanachama wa mikataba kama vile Mkataba wa Marufuku ya Uzalishaji na Matumizi ya Silaha za Kemikali. Marekani na serikali za Ulaya hutumia mikataba kama vile Mkataba wa Marufuku ya Uzalishaji na Matumizi ya Silaha za Kemikali au Mkataba wa Marufuku ya Uzalishaji na Usambazajii wa Silaha za Nyuklia (NPT) kama zana ya kuendeleza malengo yao ya kutafuta ukuu.
Naibu Waziri wa Sheria wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amewaambia wajumbe wanaoshiriki katika mkutano 29 wa Kuzuia Silaha za Kemikali kwamba: Tuhuma bandia za Marekani dhidi ya mhanga mkubwa zaidi wa silaha za kemikali katika zama hizi zinakaririwa katika hali ambayo, nchi hiyo ambayo ndio mmiliki mkubwa zaidi wa silaha za kemikali, baada ya miaka mingi ya kuchelewesha na kuakhirisha mara kwa mara tarehe ya kuangamiza hifadhi yake ya silaha hizo imekuwa mkiukaji mkuu wa mkataba huu.
Marekani ina historia ya kutoheshimu mkataba huu na mwaka 2003, baada ya uvamizi wa Iraq, ilihamisha na kuharibu silaha za kemikali zilizogunduliwa nchini Iraq kwa kuchelewesha kwa miaka sita bila kutoa taarifa kwa Shirika la Kuzuia Silaha za Kemikali.
Katika masiku hayo hayo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliripoti ukiukaji wa mara kwa mara wa Marekani na washirika wake wa mkataba huo na kuzifahamisha nchi wanachama kuhusiana na ukiukaji huo. Hadi sasa Marekani bado haijatoa jibu la kuridhisha kwa maswali ya kimsingi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Katika mwaka wa 2004 na 2008, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia iliihoji Marekani kuhusiana na ukiukaji wa mkataba huo katika uwanja wa kuusaidia utawala wa Kizayuni kutengeneza silaha za kemikali na pia silaha nyingine zilizopigwa marufuku, ambazo viongozi wa serikali ya Washington katu hawajatoa majibu ya kukinaisha kwa maswali hayo.