Iran yapinga madai ya 'Troika ya Ulaya' kuhusu kadhia ya nyuklia
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amemtumia barua Katibu Mkuu wa umoja huo na Baraza la Usalama akisema kuwa tuhuma zilizotolewa dhidi ya Tehran hazina msingi wowote na zina malengo ya kisiasa. Amir Saeid Iravani ameeleza hayo kufuatia tuhuma zilizotolewa na wawakilishi wa Troika ya Ulaya dhidi ya Tehran. Troika hiyo inajumuisha Ufaransa, Uingereza na Ujerumani.
Wawakilishi wa kudumu wa Ufaransa, Ujerumani na Uingereza katika Umoja wa Mataifa wameituhumu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa haifungamani na ahadi zake kwa mujibu wa mapatano ya JCPOA na kwamba imekiuka azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama.
Amir Saeid Iravani Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran Katika Umoja wa Mataifa mjini New York ametuma barua kwa Baraza la Usalama na kwa Katibu Mkuu wa umoja huo Antonio Guterres na akiyataja madai ya Troika ya Ulaya kuwa yasiyi na msingi na ni ya upotoshaji. Amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imechukua hatua katika fremu ya haki halali zilizoorodheshwa katika vipengee vya 26 na 36 vya mapatano ya JCPOA na katika kujibu hatua ya upande mmoja ya Marekani ya kujitoa katika mapatano hayo.
Barua ya Balozi wa Iran UN imebainisha kuwa: Troika ya Ulaya imekiuka ahadi zake katika kuondoa vikwazo na imeendeleza sera zake za uhasama kwa kuweka vikwazo vipya ikiwemo vikwazo dhidi ya njia za meli za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na sekta ya anga.
Katika barua hiyo, Iravani pia ameashiria ushirikiano wa wazi na athirifu wa Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) na kusisitiza kuwa miradi ya nyuklia ya Iran inasimamiwa kikamilifu kwa mujibu wa mkataba wa NPT, na kuwa silaha za nyuklia hazina nafasi yoyote katika mfumo wa ulinzi wa Iran.
Inaonekana hatua za Ulaya zinaelekea kwenye sera ya kuongeza mashinikizo jumla dhidi ya Iran kwa lengo la kuilazimisha Tehran ikubali matakwa yasiyo ya mantiki na yasiyo ya kisheria ya Magharibi ili kuweka vizuizi dhidi ya mpango wa nyuklia wa amani wa Iran. Aidha, lengo jingine la mashinikizo hayo ni katika fremu ya mashinikizo ya Marekani na Ulaya ya kuweka vizingiti katika uwezo uwezo wa kijeshi na kiulinzi wa Iran na hatimaye kuilazimisha ibadilishe sera zake za kieneo. Troika ya Ulaya katika mwelekeo huu pamoja na Marekani ilipiga kura katika kikao cha Bodi ya Magavana ya IAEA mnamo tarehe 21 Novemba kupitisha azimio ambalo linaitaka Iran kuchukua kile kilichotajwa kuwa "hatua muhimu na za haraka" ili kutatua masuala ya mpango wa nyuklia.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hapo awali ilitangaza kuwa itatoa jibu kali dhidi ya hatua zozote za Bodi ya Magavana ya IAEA ambazo zina malengo yasiyo halali na ya kisiasa. Katika kujibu azimio hilo, Rais wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran alitoa amri ya kuchukuliwa hatua madhubuti ikiwa ni pamoja na kuzindua mfululizo wa mashinepewa mpya na za kisasa za kurutbisha madini ya urani yanayotumika kuzalisha nishati ya nyuklia.
Inaonekana kuwa nchi hizo tatu za Ulaya zimesahau kuwa hali ya mkwamo wa sasa katika suala la mpango wa nyuklia na pia hatua za Iran katika kuendeleza teknolojia na kuongeza akiba yake ya urani ni jibu la moja kwa moja la Tehran kwa hatua ya nchi hizo ya kushindwa kutumiza ahadi zao katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA na pia kujiondoa kwa Marekani katika makubaliano hayo ya nyuklia.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran chini ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ilifanya kazi kwa miaka kadhaa kutekeleza kikamilifu wajibu wake wa nyuklia ikiwa ni pamoja kupunguza shughuli zake za nyuklia; lakini Marekani katika kipindi cha urais wa Donald Trump mnamo Mei 2018 ilijiondoa kwenye JCPOA na kuanzisha vikwazo vikali zaidi dhidi ya Iran chini ya sera ya mashinikizo ya juu zaidi.
Kwa upande mwingine, kutokana na hatua ya nchi za Ulaya kushindwa kutimiza wajibu wao katika mapatano ya JCPOA, Iran ilichukua hatua tano za kupunguza majukumu yake katika mapatano hayo na kisha kuchukua hatua zaidi katika muelekeo huo ikiwa ni kutekeleza sheria iliyopitishwa na Majlisi ya Ushauri wa Kiislamu yaani Bunge la Iran.
Miongoni mwa mambo yanayoweza kutajwa katika hatua hizo ni kuongeza urutuvbishaji wa madini ya urani hadi kiwango cha asilimia 20 na kisha asilimia 60, uzalishaji wa metali ya urani na upanuzi wa vituo na vifaa vya nyuklia, jambo ambalo limeibua kile kinachodaiwa kuwa ni wasiwasi wa Marekani na washirika wake wa Ulaya na kikanda, hasa utawala wa Kizayuni.
Jambo muhimu ni kwamba Troika ya Ulaya, licha ya ahadi nyingi ilizotoa baada ya Marekani kujiondoa katika mapatano ya JCPOA, si tu kuwa haikujaribu kupunguza madhara ya vikwazo vya upande mmoja vya nchi hiyo dhidi ya Iran, bali kwa kipindi cha urais wa Joe Biden imekuwa mshirika wa karibu wa Marekani katika kuimarisha mashinikizo dhidi ya Iran, na hii inaonyesha kuwa nchi za Ulaya zinaendelea kuvunja ahadi zao katika uwanja huo.
Wakati huo huo, inaonekana kuwa nchi za Ulaya sasa zinajitayarisha kufuata sera za rais mteule wa Marekani Donald Trump ambaye ameahidi kuendeleza kile anachodai ni mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Iran.