Safari ya Zarif Nigeria: Abuja na Tehran zasisitiza kuimarisha ushirikiano
Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Nigeria wamesisitiza juu ya azma ya nchi zao ya kuimarisha zaidi ushirikiano wa pande mbili katika nyanja mbalimbali.
Dakta Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran na mwenzake wa Nigeria, Geoffrey Onyeama, wamesisitiza hayo katika mazungumzo yao mjini Abuja, Nigeria na kubainisha kwamba, nchi hizo zimeazimia kupanua ushirikiano wao katika nyanja mbalimbali zikiwemo za kiuchumi na kisiasa.
Dakta Muhammad Javad Zarif aliwasili Abuja jana usiku akiuongoza ujumbe wa ngazi za juu wa kisiasa na kiuchumi wa Iran, ikiwa ni kituo chake cha kwanza katika safari yake ya kuzitembelea nchi kadhaa za Afrika Magharibi.
Mbali na Nigeria, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran atazitembelea pia nchi za Ghana, Guinea-Conakry na Mali.
Lengo la safari hiyo ni kufanya juhudi za kuimarisha zaidi ushirikiano kati ya Iran na nchi za magharibi mwa Afrika.
Wakati huo huo, akizungumza leo katika kikao cha ushirikiano wa kiuchumi cha Iran na Nigeria mjini Abuja, Dakta Zarif amesisitiza juu ya azma ya Tehran ya kuimarisha ushirikiano wake wa kiuchumi na Nigeria.
Dakta Zarif amesema, nchi mbili za Iran na Nigeria zina nafasi muhimu na athirifu katika asasi za kimataifa kama vileJumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM), Jumuiya ya Nchi za Kiislamu Zinazostawi D8 na Jumuiya ya Nchi Zinazozalisha Mafuta kwa Wingi Duniani (Opec).