Pezeshkian amwambia Erdogan: Unyakuzi wa ardhi ya Syria haukubaliki kwa njia yoyote
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza ulazima wa kuhifadhiwa ardhi yote ya Syria. Rais Masoud Pezeshkian ameyasema hayo katika mazungumzo yake na Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki pambizoni mwa mkutano wa viongozi wa nchi wanachama katika D-8 uliofanyika jana mjini Cairo huko Misri.
Katika mazungumzo hayo Rais Pezeshkian amesisitiza kwamba utimilifu wa ardhi ya Syria unapaswa kulindwa bila ya kudhurika hata kidogo, na amesisitiza udharura wa kusimamishwa mara moja hujuma za utawala wa Kizayuni wa Israel katika eneo la Asia Magharibi.
Pezeshkian amekumbushia wajibu wa nchi zote za Kiislamu katika uwanja huo na kusema: "Nchi za Kiislamu hazina budi kutekeleza wajibu wao katika kukabiliana na jinai na uchokozi wa utawala wa Kizayuni, na iwapo kutakuwepo umoja na mshikamano katika Umma wa Kiislamu, utawala huo hautathubutu kuchukua hatua kama hizo."
Katika sehemu nyingine ya matamshi yake, Rais Masoud Pezeshkian amezungumzia uhusiano mzuri kati ya Iran na Uturuki na mkutano wa hivi karibuni wa kamisheni ya pamoja ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili, na ametangaza utayarifu wa Iran kuandaa mkutano ujao wa Baraza Kuu la Mahusiano ya Kistratejia kati ya nchi hizo mbili.
Mwishoni, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ametoa wito wa kuimarishwa uhusiano wa kibiashara na kiuchumi baina ya nchi za Kiislamu kwa kutilia maanani uwezo mkubwa wa nchi hizo.
Kwa upande wake, Rais wa Uturuki amezungumzia umuhimu wa kudumisha amani na kulindwa ardhi yote ya Syria na kueleza matumaini yake kuwa utulivu na usalama vitaimarishwa nchini Syria haraka iwezekanavyo kwa ushirikiano wa Iran na Uturuki.
Pia, ametangaza uungaji mkono wake kwa usitishaji vita nchini Lebanon, na kusisitiza haja ya kusitishwa mashambulio ya Israel dhidi ya Syria na vita vya utawala huo katika Ukanda wa Gaza.