Mabadilishano ya kibiashara kati ya Iran na Qatar yaongezeka kwa 53%
Mabadilishano ya kibiashara kati ya Qatar na Jamahuri ya Kiislamu ya Iran yameongezeka kwa kasi katika kipindi cha miezi michache iliyopita.
Hayo yameelezwa na mwambata wa kibiashara wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Qatar ambaye sambamba na kuashiria kuchukua wigo mpana ushirikiano wa kibiashara kati ya Iran na Qatar ametangaza ongezeko la asilimia 53 la biashara kati ya nchi hizo mbili katika kipindi cha miezi 9 iliyopita.
Abbas Abdulkhani, mwambata wa kibiashara wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Qatar, akitegemea data na ripoti ya Shirika la Forodha la Iran, ametangaza kuwa, kiwango cha biashara kati ya Iran na Qatar katika kipindi cha miezi 9 iliyopita kilifikia takriban dola milioni 265 na kusema: Idadi hii ni sawa na ongezeko la 53% ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.
Akiorodhesha bidhaa muhimu zaidi za mauzo ya Iran kwenda Qatar, Abdulkhani alibainisha: Matunda na mbogamboga, mazao ya kilimo, chakula, mayai, kamba, zafarani, mazulia, vifaa vya ujenzi na madini ni miongoni mwa bidhaa muhimu zaidi Iran zilizouzwa nchini Qatar. Amesema, hii inaonyesha anuai kwa anuani ya bidhaa za Iran zisizo za mafuta zinazosafirishwa nje ya nchi.
Abdul Khani ameeleza kuwa, ongezeko kubwa la mabadilishano ya kibiashara kati ya Iran na Qatar linaonyesha uwezo wa kiuchumi wa nchi hizo mbili, jambo ambalo linaweza kupelekea ukuaji zaidi wa maingiliano ya pande mbili iwapo mazingira yataboreshwa zaidi na kuondolewa vizingiti vya kibiashara.