Pezeshkian: Mataifa ya Kiislamu yaungane kuijenga upya Gaza
(last modified Sun, 09 Feb 2025 07:14:03 GMT )
Feb 09, 2025 07:14 UTC
  • Pezeshkian: Mataifa ya Kiislamu yaungane kuijenga upya Gaza

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian ametoa mwito kwa nchi za Kiislamu kuungana na kushirikiana ili kulijenga upya eneo la Ukanda la Gaza ambalo limeharibiwa kikamilifu na mabomu ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Katika mazungumzo yake na Mwenyekiti na wajumbe wa Baraza la Shura la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS), Rais Pezeshkian ametoa mwito wa kuundwa muungo wa kimataifa wa nchi za Kiislamu kwa ajili ya kuijenga upya Gaza.

"Nchi za Kiislamu bila shaka zitaweza kuijenga upya Gaza pamoja na kurejesha uhai kwa Waislamu wa eneo hili," Pezeshkian amesisitiza hayo alipokutana na wajumbe wa Baraza la Shura la HAMAS na mwenyekiti wake Muhammad Ismail Darwish jana Jumamosi hapa mjini Tehran.

Rais wa Iran amewasifu na kuwapongeza wananchi wa Palestina kwa ushindi wao dhidi ya Israel na kusema kuwa, waliuzuia utawala huo kufikia malengo yake ya kuendesha vita katika Ukanda wa Gaza.

Miundomsingi ya Gaza ilivyoharibiwa kwa mabomu ya Wazayuni

Kadhalika amesisitiza uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu kwa mrengo wa Muqawama na watu wa Gaza, na kueleza bayana kuwa, hakuna shaka mapambano hayo ya Wanamuqawama hatimaye yataibuka na ushindi mkabala wa maadui.

"Tuna uhakika wa ushindi wa mwisho wa kambi ya Muqawama, kama Mwenyezi Mungu alivyoahidi katika Quran Tukufu," amesisitiza Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.