China na Russia zahimiza kuhitimishwa 'vikwazo haramu' dhidi ya Iran
(last modified Fri, 14 Mar 2025 14:47:16 GMT )
Mar 14, 2025 14:47 UTC
  • China na Russia zahimiza kuhitimishwa 'vikwazo haramu' dhidi ya Iran

Wanadiplomasia wa China na Russia wametoa wito wa kuondolewa "vikwazo visivyo halali" dhidi ya Iran, wakisisitiza kuwa Tehran inayo haki ya kutumia nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani.

Katika mazungumzo kati ya China, Russia na Iran mjini Beijing leo Ijumaa, wanadiplomasia wanaoziwakilisha nchi hizo tatu wamebadilishana mawazo kuhusu miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia ya Iran na masuala mengine ya kimataifa.

Wanadiplomasia hao wamesisitiza katika taarifa yao ya pamoja umuhimu wa kuondolewa vikwazo haramu na vya upande mmoja. 

Mkutano huo ulioongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Ma Zhaoxu, ulihudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Kazem Gharibabadi na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergei Ryabkov.

Wanadilplomasia hawa wa Iran, China na Russia wamekutana mjini Beijing, China ikiwa zimepita siku kadhaa baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kuitumia Iran barua akitaka kufanya mazungumzo na Iran. 

China, Russia na Iran zimesisitiza udharura wa kufanyika mazungumzo kwa msingi wa kuheshimiana pande mbili. 

Wakati huo huo Beijing na Moscow zimesisitiza kuwa zinaunga mkono matamshi ya Iran kwamba miradi yake ya nyuklia inafanyika kwa malengo ya kiraia na si kwa ajili ya kuunda silaha za nyuklia.