Qalibaf: Utawala wa Kizayuni ni mtambo wa mauaji wa Marekani mtendajinai
(last modified Sat, 29 Mar 2025 03:13:22 GMT )
Mar 29, 2025 03:13 UTC
  • Qalibaf: Utawala wa Kizayuni ni mtambo wa mauaji wa Marekani mtendajinai

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran amesema: "Utawala wa Kizayuni wa Israel ni mashine ya mauaji ya Marekani mtendajinai."

Mohammad Baqer Qalibaf, aliyasema hayo jana Ijumaa mjini Tehran katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds na kuongeza kuwa: Mfumo wa kibeberu unadumisha uhai wake kupitia dhulma na ukandamizaji dhidi ya jamii ya binadamu, na kwamba Palestina ni dhamiri iliyoamka ya jamii ya kimataifa dhidi ya mfumo wa kibeberu.

Huku akieleza kuwa uhusiano wa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel ni uhusiano wa ushirikiano, mapatano, uungaji mkono, na ushirika, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu amesema: "Uhusiano kati ya Uingereza na Israel pia ni uhusiano wa baba na mtoto," na kwa maneno mengine, Uingereza inataka kukamilisha mradi ambao haujakamilika iliouanzisha mwaka 1948 wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia na kuasisi Jumuiya ya Kizayuni.

Spika wa Bunge la Iran aidha amesisitiza kuwa, kambi ya Muqawama bado ina nguvu zinazohitajika kukabiliana na utawala wa Kizayuni na kuongeza: "Katika mazungumzo kati ya Muqawama na utawala wa Kizayuni, kila mtu aliona kwamba baada ya kuachiliwa huru mahabusi wa Kipalestina kutoka katika magereza ya Israel, mateka wa Kizayuni waliachiliwa huru, na wakati utawala wa Kizayuni ulipokiuka makubaliano ya kusitisha vita kama ilivyokuwa miaka ya huko nyuma, kambi ya Muqawama imejibu mapigo kutokea Gaza an Yemen."

Mohammad Baqer Qalibaf

Katika sehemu nyingine ya matamshi yake, Mohammad Baqer Qalibaf ameeleza kuwa, kufanya mazungumzo chini ya vitisho kuna maana ya kulazimisha matakwa yako kwa wengine, na akafafanua kuwa: Wanachokitaka viongozi wa Marekani katika mazungumzo hayo ni kuipokonya silaha Jamhuri ya Kiislamu, na hakuna taifa ambalo lingekubali takwa kama hilo.

Spika wa Bunge la Iran ameionya Marekani na waitifaki wake akisema: "Iwapo wataitishia Iran ya Kiislamu, basi washirika wa Marekani katika eneo hili na kambi za kijeshi za Marekani hazitakuwa salama, sawa kabisa na ghala la baruti."