Mshauri: Ikiwa Marekani itafanya kosa, Iran itaunda silaha za Nyuklia
(last modified Tue, 01 Apr 2025 07:46:41 GMT )
Apr 01, 2025 07:46 UTC
  • Mshauri: Ikiwa Marekani itafanya kosa, Iran itaunda silaha za Nyuklia

Mshauri mwandamizi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, iwapo Marekani itafanya 'kosa' lolote, Iran italazimika, kwa mashinikizo ya wananchi wake, kuelekea kwenye uundaji wa silaha za nyuklia.

Katika siku za hivi karibuni, Rais wa Marekani Donald Trump, akiendeleza sera zake za chuki na tamaa ya mamlaka, ametoa vitisho dhidi ya Iran, ambavyo vimeibua hisia na majibu mbalimbali.

Kwa mujibu wa Pars Today, Ali Larijani, mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, siku ya Jumatatu usiku katika mahojiano ya televisheni ya Iran, alisema: “Kufanya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran hakutakuwa na athari ndogo. Fatwa ya Kiongozi wa Mapinduzi inasisitiza marufuku ya kuwa na silaha za nyuklia. Lakini, iwapo Marekani au Israel zitatumia kisingizio cha nyuklia kuishambulia Iran, basi Iran italazimika kuelekea kwenye utengenezaji wa bomu la nyuklia.”

Larijani, ambaye pia ni mwanachama wa Baraza la Kuainisha Maslahi ya Taifa ya Iran, aliongeza kuwa: “Mpango wa nyuklia wa Iran hauwezi kuharibiwa kwa mabomu. Teknolojia ya nyuklia ya Iran imeundwa kwa njia ambayo hata baada ya mashambulizi ya mabomu, haitaathiriwa wala kucheleweshwa.”

Kuhusu barua ya hivi karibuni ya Trump kwa Iran, Larijani amesema: “Yaliyomo katika barua hiyo ni sawa tu na maneno ambayo amekuwa akiyakariri. Kauli za Marekani hazina usahihi kwa sababu zinawaletea matatizo. Wanasiasa wengi duniani huziona kauli za Trump kama propaganda tu.” 

Akiashiria kuwa Trump ndiye aliyesababisha kuvunjika kwa makubaliano ya nyuklia ya Iran na madola sita makubwa duniani yanayojulikana kwa kifupi kama JCPOA, Larijani amesema kuwa: “Mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja hufanyika ili kuelewa madai na matarajio ya pande zote.”

Larijani pia amesema kuwa: “Iran sasa ina nafasi ya kipekee miongoni mwa mataifa yenye nguvu, na nchi nyingi za Magharibi zinapenda kuwa na uhusiano huru na Iran, lakini zinashindwa kuchukua msimamo wa wazi kwa sababu ya mashinikizo ya Marekani.”

Kuhusu nafasi ya utawala wa Israel katika eneo la Asia Magharibi, Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: “Bila msaada wa Marekani, Israel haina uwezo wowote katika eneo hili. Utawala wa Kizayuni unalitumia suala la usitishaji mapigano kama chombo cha kisiasa, na mataifa mengi yanatambua kuwa ahadi za Israel hazina uzito wowote.”

Mshauri wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa njia pekee ya kujikinga dhidi ya mashambulizi ya Israel ni mapambano. Akiilaani vikali Marekani kwa mashambulizi yake dhidi ya Yemen, ameongeza kuwa: “Kama Wamarekani wangekuwa na busara, wasingejihusisha au kuchokoza Yemen.”