Wizara ya Ulinzi ya Iran: Chokochoko dhidi yetu zitakabiliwa na jibu madhubuti
(last modified Tue, 01 Apr 2025 10:53:09 GMT )
Apr 01, 2025 10:53 UTC
  • Wizara ya Ulinzi ya Iran: Chokochoko dhidi yetu zitakabiliwa na jibu madhubuti

Wizara ya Ulinzi ya Iran imewaonya vikali maadui kwamba, kitendo chochote cha uchokozi dhidi ya taifa hili kitakabiliwa na jibu la haraka na madhubuti.

Kwa mnasaba wa Siku ya Kitaifa ya Jamhuri ya Kiislamu (Farvardin 12) inayoadhishwa hii leo, Wizara ya Ulinzi imetoa pongezi zake kwa wananchi waaminifu na mashujaa wa Iran, hususan wafanyakazi wake wanaojitolea kila uchao.

Wizara hiyo imesisitiza dhamira yake kamili ya kuimarisha na kuvipa vikosi vya jeshi la nchi hii silaha za hali ya juu na za kisasa.

Imesisitiza kwamba, Jamhuri ya Kiislamu haitarudi nyuma kutoka kwa misingi na misimamo yake halali, ikitahadharisha pia kwamba, kitendo chochote cha uchokozi au uvamizi kitakabiliwa na jibu la haraka na nzito.

Jana Jumatatu, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei alisisitiza kuwa, iwapo maadui watafanya kitendo chochote kiovu dhidi ya Iran, bila shaka watapata pigo kubwa na la kuumiza.

Sehemu ndogo ya makombora ya balestiki ya Iran

Wakati huo huo, Iran imelaani vikali vitisho vya hivi karibuni vya Rais wa Marekani, Donald Trump, vya kuishambulia nchi hii kijeshi ambapo, imevitaja kuwa ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na misingi ya Hati ya Umoja wa Mataifa.

Balozi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa, Amir Saeid Iravani ametoa matamshi hayo katika barua iliyotumwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Rais wa Baraza la Usalama jana Jumatatu.