Rouhani: Kundi la 5+1 halitekelezi ipasavyo JCPOA
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema nchi za kundi la 5+1 hazitekelezi barabara makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).
Katika mahojiano yaliyorushwa hewani moja kwa moja jana Jumanne na televisheni ya taifa hapa nchini, Rais Rouhani alisema licha ya kwamba makubaliano hayo yamejenga anga nzuri ya kustawi uchumi wa nchi na kwamba Iran imeonyesha kujitolea kwa dhati kuyatekeleza, lakini madola sita yenye uwezo mkubwa duniani hayatekelezi wajibu wao inavyopasa kwa mujibu wa vipengee vya makubaliano hayo.
Rais wa Iran amesisitiza kuwa, kama upande wa pili ungetekeleza makubaliano hayo ya Vienna kama inavyotakiwa na kama walivyoahidi, Tehran ingetathmini kuingia katika makubaliano mengine na nchi hizo kwa maslahi yao, ya taifa hili, ya kieneo na kimataifa.
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kadhalika ameukosoa utawala wa Kizayuni na bunge la Kongresi ya Marekani kwa kuweka vizingiti katika utekelezwaji wa makubaliano hayo yaliyofikiwa Julai mwaka jana na kuanza kutekelezwa Januari mwaka huu.
Kauli ya Rouhani imejiri siku moja baada ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Khamenei kusema kuwa mapatano ya nyuklia kati ya Iran na nchi za kundi la 5+1 ni tajiriba inayoonesha kutokuwa na matunda wala faida kufanya mazungumzo na Marekani, na kwamba ukiukaji wa ahadi wa nchi hiyo umethibitisha tena udharura wa kutokuwa na imani na Wamarekani ambao daima wamekuwa wakitatiza na kuikwaza Iran kieneo na kimataifa.