Araqchi asisitiza kuimarishwa ushirikiano kati ya Iran na Algeria katika majukwaa ya kimataifa
(last modified Wed, 30 Apr 2025 11:14:50 GMT )
Apr 30, 2025 11:14 UTC
  • Araqchi asisitiza kuimarishwa ushirikiano kati ya Iran na Algeria katika majukwaa ya kimataifa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi amesisitiza umuhimu wa kuimarishwa ushirikiano kati ya Iran na Algeria katika vikao vya kimataifa na katika ngazi ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu ili kuunga mkono haki za wananchi wa Palestina.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeripoti kuwa Waziri Araqchi amejadili uhusiano wa pande mbili na matukio ya kieneo na kimataifa na mwenzake wa Algeria, Ahmed Attaf.

Katika mazungumzo hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu huko Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan pamoja na mashambulizi ya utawala huo huko Lebanon na kutoa wito wa kuongezwa ushirikiano na uratibu baina ya nchi mbili hizo za Kiislamu ili kukomesha mauaji ya kimbari ya watu wasio na ulinzi wa Palestina na kuzuia njama za kuwaondoa kwa nguvu Wapalestina katika ardhi yao.

Araqchi pia amemweleza mwenzake wa Algeria kuhusu mwenendo wa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani.

Vilevile amepongeza msimamo wa Algeria kuhusu suala la nyuklia la Iran wakati wa mkutano wa hivi karibuni wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria, Ahmed Attaf, ameeleza wasiwasi wake mkubwa juu ya sera za Israel za kuendelea kuvuruga amani na usalama wa eneo la Magharibi mwa Asia na kulaani mauaji ya watu wasio na hatia katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Amesisitiza ulazima wa nchi za Kiislamu na jamii ya kimataifa kuchukulia hatua madhubuti katika uwanja huo.