Iran yailaani Israel kwa kupiga mabomu kambi za wakimbizi Palestina
(last modified Wed, 14 May 2025 02:47:09 GMT )
May 14, 2025 02:47 UTC
  • Iran yailaani Israel kwa kupiga mabomu kambi za wakimbizi Palestina

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali mashambulizi ya hivi karibuni ya anga dhidi ya kambi za wakimbizi wa Kipalestina yaliyofanywa na utawala ghasibu wa Israel na kusababisha kuuawa shahidi na kujeruhiwa makumi ya Wapalestina wasio na hatia wakiwemo watoto wadogo.

Katika radimali yake kwa mashambulio ya mabomu dhidi ya makazi ya wakimbizi huko Jabalia na Khan Yunis yaliyofanywa na utawala wa Israel, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran, Esmaeil Baqaei jana Jumanne alitaja jinai hizo za Wazayuni kama ukiukwaji mkubwa na usio na kifani wa haki za binadamu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Ameeleza bayana kuwa, utawala huo mtenda jinai kwa mara nyingine tena umekiuka wazi kanuni na sheria za msingi za sheria za kimataifa.

Baqaei amesisitiza kuwa, jamii ya kimataifa, Umoja wa Mataifa na kila nchi ina wajibu wa kisheria na wa kimaadili  kuzuia mauaji ya halaiki huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu, na kuhakikisha sheria za kibinadamu za kimataifa zinaheshimiwa.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran, Esmaeil Baqaei

Ametoa wito wa kuharakishwa kwa kesi za kisheria katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC dhidi ya Israel na maafisa wake kwa uhalifu wa kivita, mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya binadamu.

Akionyesha mshikamano na watu wasio na ulinzi wa Palestina, Baqaei amehimiza jamii ya kimataifa na nchi za kikanda kuchukua hatua madhubuti kukomesha mara moja uvamizi wa kijeshi wa Israel.

Kadhalika amesisitiza haja ya kufikishwa haraka chakula na dawa katika Ukanda wa Gaza, kufunguliwa mashitaka kwa maafisa wa Israel waliohusika na uhalifu wa kivita, na kuondolewa kikamilifu kwa majeshi vamizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza.