Azma ya Iran na nchi tatu za Ulaya kuhusu kutumia diplomasia ya nyuklia
(last modified Sat, 17 May 2025 02:50:18 GMT )
May 17, 2025 02:50 UTC
  • Azma ya Iran na nchi tatu za Ulaya kuhusu kutumia diplomasia ya nyuklia

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Kazem Gharibabadi, amesema kuwa Iran na mataifa matatu ya Ulaya ambayo Uingereza, Ufaransa, na Ujerumani (yanayojulikana kama E3), wameazimia kutumia ipasavyo njia za kidiplomasia kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran.

Gharibabadi ametoa kauli hiyo kupitia chapisho kwenye akaunti yake ya X siku ya Ijumaa, kufuatia mkutano wake na wawakilishi wa mataifa hayo matatu yaliyomo katika makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015, maarufu kama Mpango wa Kamili wa Pamoja wa Utekelelzaji (JCPOA), uliofanyika mjini Istanbul, Uturuki. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayeshughulikia Masuala ya Kisiasa, Majid Takht-Ravanchi, pia alihudhuria mkutano huo.

Amesema kuwa wawakilishi wa Iran na wakurugenzi wa kisiasa wa E3 walibadilishana mawazo na kujadili hali ya hivi karibuni ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani kuhusu kuondolewa kwa vikwazo.

“Iran na E3 wameazimia kudumisha na kutumia kwa ufanisi diplomasia,” aliandika Gharibabadi.

Amebainisha kuwa Iran na E3 watakutana tena iwapo itahitajika ili kuendeleza mazungumzo hayo.

Katika makala iliyochapishwa katika jarida la Kifaransa Le Point, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema kuwa Iran na E3 zimefanya “mazungumzo ya awali katika ngazi ya manaibu mawaziri." Amesema mkutano huo ulikuwa mwanzo dhaifu lakini wenye matumaini.

Katika hotuba yake siku ya Jumatatu, Araghchi pia alionya kuwa matumizi mabaya ya utaratibu wa kurejesha vikwazo (snapback mechanism) hakutamaliza tu nafasi ya Ulaya katika JCPOA, bali pia kutachochea mivutano ambayo inaweza kugeuka kuwa isiyorekebishika.

Iran imefanya duru nne za mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na serikali ya Rais wa Marekani Donald Trump tangu Aprili, kuhusu mkataba mbadala wa JCPOA. Mazungumzo hayo yameelezwa kwa ujumla kuwa na maendeleo chanya na pande zote mbili.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi na mjumbe wa kikanda wa Rais wa Marekani, Steve Witkoff, ndio wanaoongoza timu za majadiliano. Mazungumzo hayo yanaratibiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Sayyid Badr Albusaidi.

Iran sasa inataka kuhakikisha kuwa Marekani itaondoa vikwazo vyote na haitajitoa tena kwa upande mmoja katika makubaliano hayo mapya.