Waziri Mkuu wa Pakistan apongeza jitihada za Iran kupunguza mvutano na India
Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, amesifu juhudi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kusaidia kupunguza mvutano kati ya Islamabad na New Delhi kufuatia shambulizi la kigaidi lililotokea mwezi uliopita katika eneo la Kashmir linalosimamiwa na India. Ametilia mkazo umuhimu wa kutafuta suluhu kupitia majadiliano na mikakati ya kisiasa.
Katika mazungumzo ya simu na Rais wa Iran,Masoud Pezeshkian, yaliyofanyika siku ya Jumamosi, Waziri Mkuu Sharif amebaini shukrani zake kwa juhudi “zenye huruma, mshikamano na udugu” zilizofanywa na Iran katika kusaidia kuondoa hali ya kutoelewana na kuweka mazingira ya kusitisha mapigano kati ya Pakistan na India.
Sharif pia ameifu ziara ya hivi karibuni ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran nchini Pakistan, akitambua pendekezo la Iran la kusitisha mapigano kuwa ni hatua “ya maana na iliyokuwa na mchango chanya” katika kupunguza joto la mvutano baina ya mataifa hayo mawili.
Akizungumzia historia ya mivutano, Sharif alibainisha kuwa katika kipindi cha miongo kadhaa, Pakistan na India zimeingia vitani mara tatu, lakini hakuna vita yoyote kati ya hizo iliyoleta suluhu ya kudumu kwa masuala ya msingi yanayozikabili nchi hizo mbili zenye silaha za nyuklia.
Waziri Mkuu huyo amesisitiza kuwa Pakistan inaamini kwamba migogoro kama ule wa Kashmir, vitisho vya ugaidi, na tofauti nyingine za kidiplomasia kati ya Pakistan na India, vinaweza kutatuliwa tu kwa njia ya mazungumzo na maridhiano ya kisiasa.
Akiwa na matumaini ya kuimarika kwa amani ya kudumu, Sharif amekaribisha hali ya utulivu iliyojitokeza, kuendelea kwa sitisho la mapigano, na harakati za kuleta mshikamano wa kijirani. Amempongeza Rais Pezeshkian kwa mchango wake mkubwa katika kurahisisha mchakato huu wa kidiplomasia wenye tija.
Aidha, Sharif ameelezea matarajio yake ya kuitembelea Tehran katika siku za usoni kwa mazungumzo ya kirafiki na Rais wa Iran, ili kubadilishana mawazo kuhusu masuala ya pamoja na yale yanayoathiri eneo la kanda kwa ujumla.
Kwa upande wake, Rais Pezeshkian amebainisha kuridhishwa kwake na kusitishwa kwa mapigano kati ya Pakistan na India kufuatia mapigano makali yaliyodumu kwa siku kadhaa.
Pezeshkian amesisitiza msimamo wa Iran kuwa vita na matumizi ya nguvu hayawezi kamwe kuwa suluhisho la matatizo, bali huzidisha machungu na mateso kwa mataifa husika. Amesema njia endelevu ya kushughulikia tofauti ni kupitia mazungumzo na ushirikiano wa kidiplomasia, si migogoro wala umwagaji damu.
Aidha amesisitiza kwamba ugaidi ni changamoto kuu kwa eneo zima na kuongeza kuwa kukabiliana na tishio hili la pamoja kunahitaji mshikamano, ushirikiano wa karibu, na udugu miongoni mwa mataifa ya ukanda huu.