UNHCR yaipongeza Iran kwa kuhudumia vyema wakimbizi
Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa wa (UNHCR) ameipongeza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuhudumia vyema wakimbizi.
Filippo Grandi ametoa pongezi hizo na kuthamini mchango wa Iran katika kuhudumia wakimbizi katika mazungumzo yake na Waziri wa Afya, Tiba na Elimu ya Tiba wa Iran, Mohammad-Reza Zafarqandi pambizoni mwa Mkutano Mkuu wa 78 wa Shirika la Afya Duniani mjini Geneva Uswisi.
Katika kikao hicho Grandi ameshukuru huduma zenye thamani zinazotolewa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa wakimbizi katika nyanja mbalimbali za afya, elimu na ajira na kuongeza kuwa: Licha ya vikwazo na baadhi ya matatizo ya kiuchumi, lakini huduma hizo zenye thamani kubwa za Iran ni zenye thamani kubwa na za kuthaminiwa sana.
Katika mkutano huo, Waziri wa Afya, Tiba na Elimu ya Tiba wa Iran, Mohammad Reza Zafarqandi alisisitiza: Kulinda afya ya wakimbizi ni jukumu la kimataifa, ambalo bila shaka halipaswi kuelekezwa tu kwa nchi inayowapokea.
Mohammad-Reza Zafarqandi ameongeza kuwa: Mbinu mwafaka za kifedha na kiutendaji zinapaswa kubuniwa na kuimarishwa katika ngazi ya dunia kwa ajili ya nchi zinazohifadhi wakimbizi hususan Iran.
Kwa mujibu wa ripoti, Filippo Grandi, Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) atazuru Tehran katika siku za usoni.
Mkutano wa 78 wa kila mwaka wa kimataifa wa Shirika la Afya Duniani (WHO) wenye kauli mbiu "Dunia Moja kwa Afya" ilianza Mei 19 huko Geneva na unatarajiwa kuendelea hadi tarehe 27 mwezi huu wa Mei.