Iran yaikosoa Magharibi kwa uingiliaji wa masuala ya ndani ya nchi
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni wa Iran amekosoa hatua ya nchi za Magharibi ya kuipaka matope Jamhuri ya Kiislamu kwa hatua yake ya kutekeleza hukumu ya kifo dhidi ya magaidi hapa nchini.
Bahram Qassemi amesema msimamo huo ni wa kindumakuwili na ni ithibati tosha kwamba nchi za Magharibi kwa mara nyingine tena zinaingilia masuala ya ndani ya Iran.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema badala ya nchi hizo kuwasilisha mikakati ya kuyatokomeza makundi ya kigaidi na kitakfiri katika eneo na kote duniani kwa ujumla, yanakimbilia kukashifu hukumu dhidi ya magaidi hao badala ya kuangalia jinai walizozitenda. Amesisitiza kuwa, Iran ni muhanga mkubwa wa harakati za kigaidi na kwamba serikali ya Tehran haitoruhusu makundi hayo ya kigaidi kuhatarisha usalama wake.
Kauli hii ya Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ni radiamali kwa matamshi ya hivi punde ya Zeid Ra'ad al-Hussein, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ambaye amekosoa hatua ya vyombo vya sheria nchini kutekeleza hukumu ya kunyongwa magaidi 20 na kudai kuwa hukumu hizo 'sio za kiuadlifu'. Aidha Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya alieleza wasi wasi wake juu ya kutekelezwa hukumu hiyo ya vyombo vya mahakama hapa nchini.
Juni 20, Wizara ya Usalama ya Iran ilitoa taarifa kuhusu njama iliyofeli ya magaidi wakufurishaji kutaka kutekeleza hujuma za mabomu nchini katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambapo makumi ya magaidi hao walitiwa mbaroni.