Iran yaonya italipiza kisasi iwapo IAEA itapitisha azimio dhidi yake
Iran imeonya kuwa itachukua hatua za kulipiza kisasi endapo Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) itapitisha azimio dhidi yake katika kikao chake cha leo Jumatatu.
Hiyo ni kauli ya Msemaji wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI), Behrouz Kamalvandi.
Katika mahojiano na televisheni ya taifa, alipoulizwa kuhusu msimamo wa Tehran iwapo azimio hilo litapitishwa Kamalvandi amesema:“Matarajio yoyote kutoka kwa IAEA kuhusu kuendelea kwa ushirikiano mpana na wa kirafiki kutoka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hayataweza kutimizwa."
Kamalvandi amefafanua kuwa Iran tayari imewahi kutoa onyo kabla ya kupitishwa maazimio dhidi yake miaka ya nyumba na wakati indhari yake haikuzingatiwa matokeo yake yalikuwa ni pamoja na kuongezeka mara saba uzalishaji wa urani iliyorutubishwa kwa kiwango cha asilimia 60.
Aidha, amesema kuwa Tehran tayari imeandaa orodha ya hatua itakazochukua iwapo azimio hilo litapitishwa katika kikao hicho cha leo.
Amesisitiza kuwa Iran haijawahi kurutubisha urani kwa kiwango kinachozidi asilimia 60, na kwamba ongezeko la muda mfupi lililotokea lilisababishwa na changamoto za kiufundi.
Kulingana na Kamalvandi, mataifa ya Ulaya yanajaribu kushinikiza kupitishwa kwa azimio hilo kwa lengo la kuanzisha tena utaratibu wa vikwazo vya Umoja wa Mataifa (snapback mechanism) dhidi ya Iran katika miezi ijayo.
Inaripotiwa kuwa, nchi tatu za Ulaya, yaani Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zimeandaa rasimu ya azimio itakayowasilishwa mbele ya Bodi ya Magavana ya IAEA. Hili linaweza kufungua njia ya kurejeshwa vikwazo vyote vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran chini ya makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015, kabla ya muda wa utaratibu huo kumalizika mwezi Oktoba.
Iwapo azimio hilo litapitishwa, huenda likatatiza zaidi mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja ya nyuklia kati ya Iran na Marekani. Tehran tayari imesema kuwa haitasita kuchukua hatua kali endapo vikwazo vitarejeshwa.
Katika chapisho la Ijumaa kupitia akaunti yake ya X (zamani Twitter), Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, aliitahadharisha Uingereza, Ufaransa na Ujerumani dhidi ya kile alichokiita “hatua mbaya” ya kuandaa azimio hilo, akisisitiza kuwa ni “kosa la kimkakati.”