Shamkhani asisitiza ushirikiano wa kistratejia kati ya Iran na Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i12739-shamkhani_asisitiza_ushirikiano_wa_kistratejia_kati_ya_iran_na_afghanistan
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesisitiza udharura wa kuendelezwa mazungumzo ya kiusalama kati ya Tehran na Kabul ili kupata njia ya kudumu ya kurejesha amani katika mipaka ya pamoja na kupambana na ugaidi.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Aug 06, 2016 08:53 UTC
  • Shamkhani asisitiza ushirikiano wa kistratejia kati ya Iran na Afghanistan

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesisitiza udharura wa kuendelezwa mazungumzo ya kiusalama kati ya Tehran na Kabul ili kupata njia ya kudumu ya kurejesha amani katika mipaka ya pamoja na kupambana na ugaidi.

Ali Shamkhani amesisitiza kuwa Iran iko tayari kuandaa stratejia ya pamoja katika nyanja za kisiasa, kiusalama, kiuchumi na kimipaka na Afghanistan. Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ameyadokeza hayo leo katika mazungumzo aliyofanya hapa Tehran na Muhammad Hanif Atmar, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Afghanistan. 

Ali Shamkhani akizungumza na Muhammad Hanif Atmar mjini Tehran
 

Shamkhani ameeleza masikitikio yake  na kutoa mkono wa pole kufuatia miripuko ya kigaidi iliyosababisha vifo vya watu kadhaa hivi karibuni huko Afghanistan na kubainisha kuwa kueneza machafuko kupitia njia ya kuzusha mizozo ya kidini na ugaidi ni siasa kongwe ambazo zimekuwa zikitekelezwa na baadhi ya madola ili kudhoofisha nguvu ya kitaifa na nafasi muhimu ya nchi za Kiislamu.

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ameashiria kuongezeka hali ya mchafukoge inayotokana na kuweko vikosi vya askari wa nchi za nje huko Afghanistan na pia kushtadi tatizo la usalama nchini humo na kuongeza kuwa, mchakato wa kuzidisha uwezo wa vikosi vya ulinzi vya Afghanistan katika kulinda usalana na kurejesha hamani nchini humo ni hatua inayopasa kupongezwa na ni ishara ya wazi kuwa Afghanistan inazidi kujiimarisha katika kurejesha usalama nchini. 

Katika mazungumzo hayo Muhammad Hanif Atmir, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Afghanistan amepongeza na kushukuru nafasi muhimu ya Iran katika ustawi na maendeleo ya Afghanistan na kueleza kuwa, mapambano ya pande zote dhidi ya makundi yenye misimamo ya kufurutu ada na ugaidi yanawezekana iwapo nchi zote zitashirikiana katika masuala ya usalama.