Iran: Marekani lazima ifidie makosa yake kabla ya mazungumzo
-
Seyyed Abbas Araghchi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mheshimiwa Seyyed Abbas Araghchi, amesema kuwa Tehran iko wazi kurejea kwenye meza ya mazungumzo na Marekani kwa msingi wa kuheshimiana pande zote.
Katika mahojiano ya kina na gazeti la Le Monde la Ufaransa yaliyochapishwa Alhamisi, Araghchi amesisitiza kuwa Marekani inapaswa kwanza kubadilisha mwenendo wake na kutoa dhamana kuwa haitafanya tena mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran wakati mazungumzo yakiendelea.
Ameweka wazi kuwa Iran siku zote imekuwa ikijitokeza katika mazungumzo kwa misingi ya heshima, mantiki, na ushirikiano wa kweli, akisema: "Mawasiliano ya kidiplomasia yamekuwa yakiendelea kwa njia mbalimbali. Kwa sasa kunaanzishwa njia ya mawasiliano ya moja kwa moja kupitia nchi rafiki au wapatanishi."
Araghchi alieleza kuwa: "Diplomasia ni barabara ya pande mbili. Ni Marekani iliyositisha mazungumzo na kuchagua njia ya mabavu. Hivyo basi, ni muhimu kwa Marekani kufidia makosa yake na kuonesha mabadiliko ya kweli katika mienendo yake. Tunahitaji hakikisho kuwa Marekani haitatumia nguvu za kijeshi wakati wa mazungumzo yajayo."
Amebainisha kuwa mashambulizi ya Marekani yamesababisha uharibifu kwa miundombinu ya nyuklia ya Iran, akisisitiza kuwa Iran ina haki ya kudai fidia baada ya tathmini kamili kufanyika.
Araghchi amesisitiza kuwa mpango wa nyuklia wa Iran uko chini ya usimamizi wa mara kwa mara wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), na unatekelezwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa — jambo linaloonesha kuwa mpango huo ni zaidi ya miundombinu tu ya vifaa.
Amebaini kuwa ripoti za IAEA zimeendelea kuthibitisha kuwa hakuna ushahidi wowote wa mwelekeo wa kijeshi katika mpango wa nyuklia wa Iran."
Araghchi ametoa hakikisho kuwaIran haina nia ya kujiondoa kutoka Mkataba wa Kuzuia Usambazaji wa Silaha za Nyuklia (NPT), na itaendelea kuuheshimu, lakini akasisitiza kuwa mkataba huo haupaswi kutekelezwa kwa upendeleo au kwa upande mmoja tu.