Bunge: Marekani itimize masharti ya Iran iwapo inataka kuendelea na mazungumzo
Bunge la Iran limetoa taarifa na kutangaza kwamba, Jamhuri ya Kiislamu katu haiwezi kufanya mazungumzo na Marekani kama ilivyokuwa kabla ya uchokozi wa hivi karibuni, na kwamba hakuna mazungumzo mapya na Marekani yanapaswa kufanyikakabla ya masharti ya Tehran kutimizwa.
Taarifa hiyo, ikirejelea uvamizi wa kijeshi wa siku 12 wa Marekani na Israel dhidi ya Iran, imeishutumu Washington kwa kutumia diplomasia kama "chombo cha udanganyifu" kuficha uvamizi wa Israel.
Taarifa hiyo imesema Marekani ina hatia ya "hatua chafu na uhalifu mkubwa" kwa kushirikiana na serikali za Ulaya na Israel, kwa lengo la kuisambaratisha Iran na kutoa pigo kwa Jamhuri ya Kiislamu.
Wabunge hao wamesisitiza kuwa, mazungumzo yoyote yajayo ni lazima yazingatie dhamana ya kutovamiwa Iran na hakikisho kamili la usalama wa taifa hili. "Marekani inapotumia diplomasia kama chombo cha kuihadaa Iran na kuficha uvamizi wa kijeshi wa ghafla wa utawala wa Kizayuni, mazungumzo hayawezi tena kuendelea kama hapo awali. Masharti lazima kuwekwa na hakuna mazungumzo mapya yanapaswa kufanywa kabla ya kufikiwa kikamilifu." Imesema Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran).
Taarifa hiyo pia imesisitiza hatua ya Bunge kusimamisha ushirikiano na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, ikieleza ushiriki wa wakala huo katika kuhalalisha mashambulio dhidi ya wanasayansi wa nyuklia wa Iran na miundombinu ya nyuklia.
"Serikali ya kichokozi ya Marekani na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, ambayo ilihalalisha uchokozi huu, lazima ijue kwamba hadi Iran ipate uhakikisho kamili wa kutovamia tena, haitatoa taarifa yoyote kwa majasusi na wavamizi."
Kadhalika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu imesifu uhamasishaji na Muqawama wa watu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kukabiliana na uchokozi.