Velayati na Nouri al-Maliki wasisitiza kuungwa mkono Kambi ya Muqawama
Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Masuala ya Kimataifa amefanya mazungumzo ya simu na Waziri Mkuu wa zamani wa Iraq, Nouri al-Maliki ambapo pande hizo mbili zimejadili matukio ya kikanda na kusisitiza udharura wa kuungwa mkono Kambi ya Muqawama.
Pande hizo mbili zimebadilishana mawazo kuhusu matukio ya hivi karibuni katika eneo la Asia Magharibi hususan njama mpya za utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani dhidi ya Muqawama wa Kiislamu.
Akigusia hatua za hivi karibuni za Marekani na Wazayuni za kutaka kudhoofisha Kambi ya Muqawama, Velayati amesisitiza kuwa: "Mwenyezi Mungu akipenda, kwa msaada wa mihimili yote ya Mapambano, tutasimama dhidi ya Marekani na utawala wa Kizayuni na hatutaruhusu malengo yao maovu yatimie."
Kwa upande wake, Nouri al-Maliki ametahadharisha kuhusu hali nyeti ya eneo hilo na kusema: "Leo tunashuhudia kwamba wana nia ya kuipokonya silaha Hizbullah nchini Lebanon, na bila shaka, hatua itakayofuata itakuwa zamu ya Iraq, vikosi vya al Hashdul Shaabi na makundi mengine ya mapambano. Hatutaruhusu mipango hiyo kutekelezwa kwa hali yoyote ile, na tutasimama dhidi yake pamoja na Kambi ya Muqawama."
Katika mazungumzo hayo, pande hizo mbili zimesisitiza kuwa, fikra ya kupokonywa silaha Hizbullah ya Lebanon na vikosi vya al Hashdul Shaabi nchini Iraq ni sehemu ya mpango wa Wamarekani na Wazayuni wa kudhoofisha Muqawama na mapambano, na mataifa ya eneo hili hayapaswi kuruhusu utekelezaji wa mradi huo hatari.