Iran yaionya Ulaya juu ya matokeo mabaya ya kuamilisha 'snapback'
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i129880-iran_yaionya_ulaya_juu_ya_matokeo_mabaya_ya_kuamilisha_'snapback'
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi ameionya Ulaya juu ya matokeo mabaya ya kuamilisha "utaratibu wa snapback", akisisitiza kwamba Troika ya Ulaya (Uingereza, Ufaransa, na Ujerumani) pamoja na Umoja wa Ulaya hazina haki ya kisheria na ya kimaadili ya kutumia utaratibu huo.
(last modified 2025-08-23T06:16:25+00:00 )
Aug 23, 2025 06:16 UTC
  • Iran yaionya Ulaya juu ya matokeo mabaya ya kuamilisha 'snapback'

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi ameionya Ulaya juu ya matokeo mabaya ya kuamilisha "utaratibu wa snapback", akisisitiza kwamba Troika ya Ulaya (Uingereza, Ufaransa, na Ujerumani) pamoja na Umoja wa Ulaya hazina haki ya kisheria na ya kimaadili ya kutumia utaratibu huo.

Araghchi aliyasema hayo katika mazungumzo yake ya Ijumaa kwa njia ya simu na mwakilishi mkuu wa sera za mambo ya nje na usalama wa Umoja wa Ulaya na mawaziri wenzake wa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, nchi tatu zilizotia saini makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015, JCPOA.

Katika mazungumzo hayo, Araghchi ameashiria misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu kile kinachoitwa utaratibu wa snapback na kufafanua majukumu ya nchi tatu za Ulaya na EU katika muktadha huu.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amesisitiza kuwa, ingawa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imechukua hatua madhubuti za kujilinda, lakini imekuwa ikifuata njia za kidiplomasia na bado iko wazi kwa suluhisho lolote la kidiplomasia linalolinda haki na maslahi ya watu wa Iran.

Snapback au trigger mechanism ni mchakato kurejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Sayyid Araghchi amewatahadharisha wakuu wa Ulaya katika makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 kwamba, kutumia "snapback" ni kinyume cha sheria, lakini Tehran imejiandaa kutoa majibu kwa jaribio lolote la kurejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya nchi hiyo.

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Russia, Abbas Araghchi na Sergei Lavrov

Wakati huo huo, Iran na Russia zimesisitiza kwamba, Troika ya Ulaya, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani hazina haki ya kujaribu kulifanya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) kurejesha vikwazo vyake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Wanadiplomasia wakuu wa nchi hizo mbili, Abbas Araghchi na Sergei Lavrov, walisema hayo katika mazungumzo ya simu jana Ijumaa na kusisitiza kuwa, Ulaya haina mamlaka ya 'kisheria, kimaadili' ya kuamilisha utaratibu wa 'snapback'.