Iran na Ulaya kuendelea na mazungumzo ya nyuklia mjini Geneva
Iran na nchi tatu zenye nguvu za Ulaya - Ujerumani, Ufaransa na Uingereza - zinatazamiwa kuanza tena mazungumzo ya nyuklia huko Geneva, Uswisi siku ya Jumanne, yakiangazia maswala ya nyuklia na uondoaji wa vikwazo.
Kwa mujibu wa chanzo chenye ufahamu wa mazungumzo hayo kilichozungumza na shirika la habari la Tasnim, Iran na nchi tatu za Ulaya (Ujerumani, Ufaransa, na Uingereza) zimeafikiana kuanza tena mazungumzo ya nyuklia mjini Geneva kesho.
Chanzo hicho kimesema, ajenda ya mazungumzo hayo itahusu masuala ya nyuklia na kuondolewa Jamhuri ya Kiislamu ya Kiislamu ya Iran vikwazo haramu.
Tasnim imeripoti kwamba, Majid Takht-Ravanchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ataongoza ujumbe wa Jamhuri ya Kiislamu mjini Geneva, wakati manaibu mawaziri wa mambo ya nje wataziwakilisha Ujerumani, Ufaransa na Uingereza.
Haya yanajiri huku Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi akiionya Ulaya juu ya matokeo mabaya ya kuamilisha "utaratibu wa snapback", akisisitiza kwamba Troika ya Ulaya (Uingereza, Ufaransa, na Ujerumani) pamoja na EU hazina haki ya kisheria na ya kimaadili ya kutumia utaratibu huo.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amesisitiza kuwa, ingawaje Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imechukua hatua madhubuti za kujilinda, lakini imekuwa ikifuata njia za kidiplomasia na bado iko wazi kwa suluhisho lolote la kidiplomasia linalolinda haki na maslahi ya watu wa Iran.
Wakati huo huo, Iran, China na Russia zimesisitiza kwamba, Troika ya Ulaya, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani hazina haki ya kujaribu kulifanya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) kurejesha vikwazo vyake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.