Iran yakemea mashambulizi ya Israeli dhidi ya vongozi wa Hamas jijini Doha
Iran imelaani vikali mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Israel dhidi ya viongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Ukombozi wa Palestina, Hamas, wakati walipokuwa wakijadili pendekezo la Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu kusitisha mapigano huko Gaza,ikiyataja kuwa ni ukiukaji wa misingi yote ya sheria za kimataifa.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, amesema mashambulizi hayo ya Jumanne dhidi ya makao ya Hamas katika mji mkuu wa Qatar, Doha, ni hatari sana, yanakiuka kanuni na taratibu zilizowekwa za sheria za kimataifa, na yanapingana na Hati ya Umoja wa Mataifa.
“Shambulizi hili ni hujuma dhidi ya mamlaka ya kitaifa na uhuru wa ardhi wa Qatar, pamoja na wajumbe wa Palestina waliokuwa wakijadiliana. Tukio hili linapaswa kuwa onyo kali kwa eneo zima la Asia Magharibi na kwa jumuiya ya kimataifa, ili wasiendelee kunyamaza mbele ya ukiukaji wa mara kwa mara wa sheria na uhalifu unaoendelezwa na utawala wa Kizayuni.”
Afisa mmoja mwandamizi wa Israel aliiambia televisheni ya Channel 13 ya utawala huo kuwa viongozi wa Hamas, Khalil al-Hayya na Zaher Jabarin, mwenyekiti wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas katika Ukingo wa Magharibi, walikuwepo kwenye kikao hicho kilicholengwa.
Ripoti zinaeleza kuwa kiongozi wa muda mrefu wa Hamas, Khaled Mashaal, ambaye Israel ilijaribu kumuua nchini Jordan mwaka 1997, alikuwepo pia katika mkutano huo. Taarifa zinasema viongozi hao wa ngazi za juu wa Hamas wamenusirika katika hujuma hiyo.
Afisa mwingine wa Israel ambaye hakutajwa jina aliiambia televisheni ya Channel 12 kuwa Rais Donald Trump alitoa idhini ya mashambulizi hayo ya Israel ndani ya Qatar.
Mnamo Septemba 7, Trump alitangaza kuwa amewasilisha pendekezo jipya la kumaliza vita vya Gaza, akidai kuwa Israel imekubali masharti yake. Alionya Hamas ikubali masharti hayo, akisema kuwa ameijulisha harakati hiyo kuhusu “matokeo” ya kuyakataa.
Maafisa wa Marekani wanasema Israel imekubali mipango ya kusitisha mapigano, licha ya viongozi wa Israeli kuendelea kutangaza wazi kuwa wataendeleza kampeni yao ya mauaji ya halaiki.
Hamas imethibitisha kupokea “mawazo” kutoka Marekani kuhusu kumaliza vita.
Inasadikiwa kuwa kundi hilo la kupigania ukombozi wa Palestina linawashikilia takriban mateka 50 wa Kiyahudi, ambapo 20 kati yao bado wanaaminika kuwa hai.
Wakati huohuo, Qatar imesitisha mazungumzo ya makubaliano hadi taarifa nyingine itakapotolewa, kufuatia shambulizi dhidi ya uongozi wa Hamas.