Kamanda Mousavi: Wananchi, wanajeshi wa Iran watasimama na Qatar
Mkuu wa Kamandi ya Majeshi ya Iran amesema kuwa serikali, taifa na vikosi vya kijeshi vya Qatar vinapaswa kujua kwamba, Jamhuri ya Kiislamu na jeshi lake litaendelea kusimama upande wao hadi mwisho.
Meja Jenerali Abdolrahim Mousavi amesema hayo katika mazungumzo ya simu na Naibu Waziri Mkuu wa Qatar na Waziri wa Mambo ya Nje wa Masuala ya Ulinzi Saoud bin Abdulrahman Al Thani jana Alkhamisi.
Meja Jenerali Mousavi amesema kuwa Iran inalaani vikali shambulio la utawala wa Israel katika ardhi ya Qatar, kama ilivyotangazwa na maafisa wakuu wa Iran dakika chache baada ya uvamizi huo.
Amesisitiza kuwa, jeshi la Iran halitasita kuiunga mkono Qatar akitolea mfano uhusiano wa kidugu uliopo kati ya nchi hizi mbili. Ameongeza kuwa, Iran haitaiacha Qatar mbele ya maadui zake hususan utawala wa Israel ambao ameutaja kuwa ni wa kijinai na chanzo kikuu cha mivutano na ukosefu wa amani katika eneo hili.
Aidha Mkuu wa Kamandi ya Majeshi ya Iran amesema uungaji mkono usio na masharti wa Marekani kwa uvamizi, ukandamizaji na mauaji ya watu wa Palestina na uvamizi wake katika nchi nyingine, umeushajiisha utawala wa Israel. Kadhalika amebainisha kuwa shambulio dhidi ya Qatar lisingeweza kutokea bila ridhaa ya Washington.
Qatar imeitaja hujuma hiyo ya Wazayuni wakati wa mazungumzo ya amani kuwa "mashambulio ya kigaidi". Siku ya Jumanne, ndege za kivita za Israel zilifanya mashambulizi ya anga dhidi ya Doha katika jaribio la kuwauwa viongozi wa Hamas waliokuwa wamekusanyika kuhakiki pendekezo la hivi punde la Marekani la kusitisha mapigano Gaza.
Akitoa shukrani a dhati kwa uungaji mkono wa Iran, Al Thani amesema utawala wa Israel haufuati kanuni au sheria yoyote, na kwamba tukio la hivi majuzi lilikiuka mistari yote myekundu, viwango vya kimataifa na itifaki za kidiplomasia. Ameongeza kuwa, shambulio hilo lilikuwa na nia ya kudhoofisha juhudi za Qatar za kutafuta suluhu ya amani kwa mzozo wa Gaza.