Araghchi: Iran ina azma ya kuimarisha uhusiano imara na ulimwengu wa Kiislamu
Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, amesema kuwa mahusiano kati ya Iran na Tunisia ni “mfano angavu” wa dhamira ya Tehran kuendeleza uhusiano imara na mataifa ya Kiislamu kwa msingi wa “maslahi ya pamoja na heshima kwa mamlaka ya kitaifa.”
Araghchi ametoa kauli hiyo kupitia makala yenye kichwa “Uhusiano Usioyumbika; Kuelekea Mustakabali wa Pamoja kati ya Iran na Tunisia” iliyochapishwa katika vyombo vya habari vya Tunisia, kufuatia ziara yake nchini humo ambapo alikutana na Rais Kais Saied pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje, Mohamed Ali Nafti, kujadili masuala muhimu ya pande mbili.
Kwa mujibu wa Araghchi, Tunisia ina nafasi ya “kipekee na ya juu” katika sera ya mambo ya nje ya Iran, akisisitiza kuwa uhusiano wa mataifa haya mawili, ulio na mizizi ya kihistoria, umejengwa juu ya msingi wa “undugu, kuheshimiana, maelewano ya kina ya kidini na kitamaduni, pamoja na malengo ya kimataifa ya pamoja.”
Ameeleza kuwa mahusiano hayo yameendelea kwa kasi chanya na yenye uhai, akitaja ziara ya kihistoria ya Rais Kais Saied nchini Iran mwezi Mei 2024, ambayo ilihusisha mkutano na Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, kuwa ni hatua ya kihistoria iliyofungua sura mpya ya ushirikiano wa kina.
Araghchi ameisifu Tunisia kwa msimamo wake thabiti na wa kimaadili, pamoja na msaada wake wa thamani wakati wa uvamizi wa hivi karibuni wa Israeli dhidi ya ardhi ya Iran mwezi Juni, akisema kuwa msaada huo unaonesha “kina cha uhusiano wa kindugu na mshikamano usiovunjika kati ya mataifa haya mawili.”
Iran na Tunisia, alisema, zimekuwa zikishirikiana kwa msimamo mmoja katika jukwaa la kimataifa, ikiwemo kupinga kwa nguvu uingiliaji wa mataifa ya kigeni, kuunga mkono kwa dhati suala la Palestina, na kukataa kwa pamoja juhudi za kuwa na mahusiano na Israel.
Waziri huyo wa Iran amekiri kuwa ingawa mahusiano ya kisiasa kati ya Iran na Tunisia yamekuwa chanya na yenye manufaa kihistoria, lakini bado mataifa haya hayajafaidika kikamilifu na uwezo wao mkubwa wa kiuchumi.
Araghchi ameeleza kuwa “kuimarika kwa kiwango kikubwa” biashara ya pande mbili kunahitaji “azma maradufu,” lakini akaonyesha matumaini kuwa nia thabiti ya viongozi wakuu wa mataifa haya inaashiria mustakabali mzuri wa mahusiano ya kiuchumi.
Amesema, kuimarisha ushirikiano katika sekta ya utalii kupitia kufutwa viza za pande mbili, kuanzishwa safari za moja kwa moja za ndege, na kuitishwa kwa kikao kipya cha Tume ya Pamoja ya Kiuchumi ni miongoni mwa hatua madhubuti zitakazochochea mahusiano ya kiuchumi kati ya Iran na Tunisia.
Aidha, ameeleza utayari wa Iran wa kushirikiana na Tunisia katika nyanja mbalimbali kwa kutumia uzoefu wake, maarifa ya kiteknolojia na teknolojia za asili.
Araghchi pia amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mabadilishano ya kitamaduni na kisanii, hususan katika filamu, muziki, kazi za mikono na michezo, ili kuimarisha uelewano wa pande mbili na kuendeleza mahusiano ya watu kwa watu kati ya Iran na Tunisia.