Araqchi alitaka Baraza la Usalama la UN kuchagua diplomasia badala ya makabiliano
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i131008-araqchi_alitaka_baraza_la_usalama_la_un_kuchagua_diplomasia_badala_ya_makabiliano
Abbas Araqchi Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuingilia kati na kuchagua njia ya diplomasia badala ya makabiliano.
(last modified 2025-09-23T11:30:28+00:00 )
Sep 20, 2025 02:47 UTC
  • Araqchi alitaka Baraza la Usalama la UN kuchagua diplomasia badala ya makabiliano

Abbas Araqchi Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuingilia kati na kuchagua njia ya diplomasia badala ya makabiliano.

Juzi Alhamisi Araqchi alieleza kuwa amewasilisha mpango unaofaa na unaoweza kutekelezeka kwa pande tatu za Ulaya zinazohusika katika makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 ili kuzuia mgogoro usio wa lazima na unaoweza kuepukika.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alibainisha haya kabla ya kuanza mkutano wa Baraza la Usalama ulioitishwa ili kujadili kuhuishwa utaratibu wa makubaliano kwa jina la Snapback. 

Mwenyekiti wa kiduru wa Baraza la Usalama la UN amesema kuwa baraza hilo  Ijumaa lilitazamia kupiga kura kuhusu imma kuiwekea tena vikwazo Iran kuhusiana na miradi yake ya nyuklia yenye malengo ya amani. 

Uingereza, Ufaransa na Ujerumani ndizo zilizochochea kura hiyo katika Baraza la Usalama. Nchi hizo tatu za Ulaya ambazo zilisainia makubaliano kwa jina la Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) zinadai kuwa Iran imevunja ahadi zake kwa mujibu wa makubaliano hayo ya mwaka 2015.

Araqchi ameeleza kushangazwa na hatua za Ulaya akisema kuwa nchi hizo badala ya kujihusisha na vipengele muhimu vya makubaliano hayo, Umoja wa Ulaya umekuwa ukitoa visingizio kadha wa kadha, ikiwa ni pamoja na matamshi ya ajabu kwamba Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran haiwakilishi taasisi nzima ya kisiasa.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema katika mahojiano ya televisheni ya Israel juzi Alhamisi kwamba anataraji vikwazo vya kimataifa dhidi ya Iran vitarejeshwa mwishoni mwa mwezi huu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kwa upande wake amebainisha kuwa juhudi za kidiplomasia za Troika ya Ulaya zinaonekana kutokuwa na tatahira na kusisitiza kuwa kuna ulazima kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutanguliza diplomasia badala ya makabiliano.