SNSC: Iran kusitisha ushirikiano na IAEA baada ya kuwekewa tena vikwazo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i131066-snsc_iran_kusitisha_ushirikiano_na_iaea_baada_ya_kuwekewa_tena_vikwazo
Baraza Kuu la Usalama la Taifa la Iran (SNSC) limesema Tehran itasitisha ushirikiano wake na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupiga kura ya kutoiondolea kabisa Tehran vikwazo dhidi yake.
(last modified 2025-09-21T06:54:26+00:00 )
Sep 21, 2025 06:52 UTC
  • SNSC: Iran kusitisha ushirikiano na IAEA baada ya kuwekewa tena vikwazo

Baraza Kuu la Usalama la Taifa la Iran (SNSC) limesema Tehran itasitisha ushirikiano wake na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupiga kura ya kutoiondolea kabisa Tehran vikwazo dhidi yake.

Katika taarifa yake jana Jumamosi, Taasisi hiyo kuu ya usalama ya Iran ilishutumu hatua "zisizozingatiwa" za nchi tatu za Ulaya yaani Uingereza, Ufaransa na Ujerumani  yaani Troika ya Ulaya (E3) kuhusu mpango wa amani wa nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu.

Juzi Ijumaa nchi 15 wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zilishindwa kupasisha azimio ambalo lingezuia kurejeshwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran baada ya nchi hizo tatu za Ulaya kutekeleza jaribiio la kurejeshwa vikwazo kupitia utaratibu wa Snapback zikiituhumu Tehran kuwa imeshindwa kufungamana na makubaliano ya mwaka 2015 kwa jina la JCPOA. 

Iran kwa upande wake imepinga hatua hiyo iliyo kinyume cha sheria ya Troika ya Ulaya Iran ikisema kuwa Marekani tayari imejiondoa katika makubaliano hayo na kuzituhumu nchi hizo tatu zaUlaya kwa kuegemea upande wa vikwazo vilivyo kinyume cha sheria badala ya kuheshimu ahadi zao.

Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran limejadili hali ya mambo ya sasa katika eneo hilo na hatua hatari za utawala wa Israel katika kikao cha jana kilichoongozwa na Rais Masoud Pezeshkian. 

Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran limesisitiza kuwa licha ya Wizara ya Mambo ya Nje kushirikiana na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) na kuwasilishwa mapendekezo ili kutatua kadhia ya nyuklia, lakini hatua za nchi za Ulaya zimepelekea kusimamishwa njia ya ushirikiano na wakala huo. 

Taarifa ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran imeeleza kuwa: Taasisi hiyo ya juu ya usalama ililipa jukumu Wizara ya Mambo ya Nje la kuendelea na mashauriano ndani ya mfumo wa maamuzi ya ya baraza hilo ili kulinda maslahi ya taifa.

"Sera ya mambo ya nje ya Iran katika mazingira ya sasa itaelekezwa katika ushirikiano ili kudumisha amani na utulivu katika eneo," imeongeza taarifa ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran.