Pezeshkian: Iran kamwe haitasalimu amri mbele ya mashinikizo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i131068-pezeshkian_iran_kamwe_haitasalimu_amri_mbele_ya_mashinikizo
Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuhusu msimamo thabiti wa Iran, na kusema Jamhuri ya Kiislamu itashinda vikwazo vinavyochochewa na wale wote wenye nia mbaya na kamwe haitasalimu amri mbele ya uonevu na matakwa yao ya mabavu.
(last modified 2025-09-21T06:52:40+00:00 )
Sep 21, 2025 06:52 UTC
  • Pezeshkian: Iran kamwe haitasalimu amri mbele ya mashinikizo

Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuhusu msimamo thabiti wa Iran, na kusema Jamhuri ya Kiislamu itashinda vikwazo vinavyochochewa na wale wote wenye nia mbaya na kamwe haitasalimu amri mbele ya uonevu na matakwa yao ya mabavu.

Akihutubia jana katika hafla ya kuwapongeza washindi wa medali za Olympiads za Sayansi ya Dunia za mwaka 2025  Rais Pezeshkian ameashiria kushindwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitisha rasimu ya azimio la kuondoa kikamilifu vikwazo dhidi ya Iran. Amesema, maadui hawawezi kuzuia njia ya yoyote mwenye dhamira, nia na uwezo wa kupiga hatua. 

"Hatutasalimu amri kwa sababu tunao uwezo  wa kuleta mageuzi, na  hatupasi kuuruhusu utawala bandia unaotenda jinai kulazimisha na kuzitwisha nchi nyingine matakwa yake haramu katika eneo hili.

Rais amesisitiza kuwa, serikali yake inawajibika kutekeleza marakebisho katika mfumo wa elimu kwa njia ambayo itawawezesha vijana wa Iran kuondokana na vikwazo bila kusita wanapofuatilia malengo yao.

Rais Pezeshkian amewapongeza  wote waioibuka na ushindi na kutunukiwa medali katika Mashindano ya Olympiad ya Sayansi ya Dunia mwaka huu kwa kuiletea fakhari nchi kwa kunyanyua bendera za Iran katika medani ya kimataifa. Amesema anatumai kuwa vijana wa Iran wataifikisha nchi  katika kilele cha maendeleo.