Araghchi: Israel inatumia mamilioni ya dola kulipa watu waongope mitandaoni
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i131704-araghchi_israel_inatumia_mamilioni_ya_dola_kulipa_watu_waongope_mitandaoni
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi ameshutumu kampeni ya propaganda iliyofichuliwa hivi karibuni ya Israel, yenye lengo la kuhamasisha uungwaji mkono kwa utawala huo kwenye mitandao ya kijamii.
(last modified 2025-10-07T07:20:50+00:00 )
Oct 07, 2025 07:20 UTC
  • Araghchi: Israel inatumia mamilioni ya dola kulipa watu waongope mitandaoni

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi ameshutumu kampeni ya propaganda iliyofichuliwa hivi karibuni ya Israel, yenye lengo la kuhamasisha uungwaji mkono kwa utawala huo kwenye mitandao ya kijamii.

Katika ujumbe kwenye akaunti yake ya mtandao wa X jana Jumatatu, Araghchi amesema, "Hatulipi watu kusema uwongo kwenye mitandao ya kijamii. Hivyo ndivyo Israel inafanya."

Ujumbe wa Araghchi umekuja baada ya kutolewa ripoti ya Taasisi ya Quincy, ambayo ilifichua kuwa utawala wa Israel unalipa takriban watu 14 hadi 18 wenye ushawishi mkubwa kwenye mitandao ya kijamii karibu dola 7,000 kwa kila ujumbe unaolenga 'kujenga taswira nzuri' ya Israel katika maoni ya umma nchini Marekani.

Kufichuliwa kwa ripoti hii kumejiri sanjari na kuongezeka kampeni ya kimataifa ya kususiwa, kulaaniwa na kuchukiwa Israel kutokana na mauaji ya kimbari ya utawala huo wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina huko Gaza.

Ripoti hiyo inasema kampeni ya kimataifa ya Israel yenye thamani ya shekeli milioni 545 (dola milioni 145) ya kukabiliana na ukosoaji unaoongozeka wa kimataifa dhidi yake ni pamoja na kutumia programu za Akili Mnemba AI kama vile ChatGPT, kubuni habari za kuupigia debe utawala huo wa Kizayuni.

Ikinukuu nyaraka mpya zilizowasilishwa na Wizara ya Sheria ya Marekani, Ynetnews iliripoti jana Jumatatu kwamba, Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel imezindua "moja ya kampeni zake kabambe za diplomasia ya umma" nchini Marekani tangu vita vya mauaji ya kimbari huko Gaza kuanza, huku kukiwa na wimbi kubwa la kupungua kwa uungaji mkono kwa Israel miongoni mwa vijana wa Marekani.

Kwa mujibu wa kura ya maoni ya Gallup iliyochapishwa mwezi Julai, ni asilimia 9 tu ya Wamarekani wenye umri wa miaka 18 hadi 34 wanaounga mkono vita vya Israel huko Gaza.