Iran yapanua diplomasia ya utalii katika mkutano wa Riyadh
-
Iran yapanua diplomasia ya utalii katika mkutano wa Riyadh
Waziri wa Utalii wa Iran Sayyid Reza Salehi-Amiri jana Jumapili alikutana na kuzungumza kwa nyakati tofauti mjini Riyadh, Saudi Arabia na maafisa wa ngazi ya juu wa nchi kadhaa, wakiwemo maafisa kutoka Indonesia, China, India, Iraq, Tajikistan, Armenia, na Uzbekistan kujadili njia za kupanua ushirikiano wa pande mbili katika sekta ya utalii.
Mazungumzo hayo yalifanyika pambizoni mwa Mkutano Mkuu wa Taasisi ya Utalii Duniani ya Umoja wa Mataifa (UNWTO) ambapo Salehi Amiri alitilia mkazo kuimarisha diplomasia ya utalii, mahusiano ya kiutamaduni na mabadilisho ya kisayansi na rasilimali watu.
Waziri wa Utalii wa Iran ameashiria utamaduni wa aina yake, ustaarabu na turathi za kimataduni za nchi hii na kusema: "Iran licha ya kuwa na utamaduni, hali ya hewa na historia anuwai iko tayari kuchukua hatua madhubuti za kupanua ushirikiano katika sekta ya utalii, urithi wa kitamaduni, kazi za mikono na utafiti na nchi marafiki na waitifaki wake.
Sayyid Reza Salehi-Amiri amesema taswira halisi, nzuri na ya kitamaduni ya Iran inapasa kufahamika vyema duniani kote na kwamba Wizara ya Utalii ya Iran iko tayari kuwapokea watalii kutoka nchi mbalimbali na wakati huo huo kuwatuma nje ya nchi waongoza watalii wa Kiirani na watalaamu wa masuala ya utalii.