Uchina: Tehran haitasalimu amri mbele ya mashinikizo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i137774-uchina_tehran_haitasalimu_amri_mbele_ya_mashinikizo
Huku akielezea upinzani wa Beijing kuhusu kushambuliwa miundombinu ya Iran, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, amesema Tehran kamwe haitapigishwa magoti na mashinikizo yoyote ya kijeshi na kwamba hatua hizi zitachochea tu moto wa mivutano.
(last modified 2026-04-04T02:52:13+00:00 )
Apr 04, 2026 02:52 UTC
  • Uchina: Tehran haitasalimu amri mbele ya mashinikizo

Huku akielezea upinzani wa Beijing kuhusu kushambuliwa miundombinu ya Iran, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, amesema Tehran kamwe haitapigishwa magoti na mashinikizo yoyote ya kijeshi na kwamba hatua hizi zitachochea tu moto wa mivutano.

Mao Ning, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China ameashiria shambulio la Washington kwenye daraja la raia mjini Karaj katika mkutano na waandishi wa habari na kusema: "Hatua za kijeshi za Marekani na Israel dhidi ya Iran zimetekelezwa bila ya idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na ni kinyume cha sheria za kimataifa."

Amesisitiza kuwa, China inapinga mashambulizi dhidi ya miundombinu na vituo vya kiraia na kuongeza: Vitendo hivyo haviwezi kuulazimisha upande wa pili kusalimu amri bali vitaongeza tu mivutano.

Msemaji wa chombo cha diplomasia cha China amesema: Katika hali ya hivi sasa, pande husika zinapaswa kutekeleza usitishaji vita mara moja na kurejea kwenye njia ya usuluhishaji wa kisiasa na kidiplomasia.

Mao Ning pia amesema kuhusu hali ya uchukuzi na usafirishaji katika Lango-Bahari la Hormuz na uwezekano wa China kushiriki katika ushirikiano wa kimataifa katika kudhamini usalama wa usambazaji nishati kwamba: "Pande zote zinataka kurejea haraka amani na utulivu kwenye njia hii muhimu, kwa sababu Lango-Bahari la Hormuz na maji yanayolizunguka ni mojawapo ya njia muhimu zaidi za biashara ya kimataifa ya bidhaa na nishati." Ameongeza: "Katika hali ya sasa, ufunguo wa kutatua tatizo hilo ni kusimamishwa operesheni za kijeshi haraka iwezekanavyo, na hapo ndipo tunaweza kuwa na matumaini ya kurejea utulivu katika eneo la Asia Magharibi na Ghuba ya Uajemi."