Iran yamuua kiongozi wa kundi la kigaidi lenye uhusiano na Saudi Arabia
(last modified Thu, 25 Aug 2016 15:01:33 GMT )
Aug 25, 2016 15:01 UTC
  • Iran yamuua kiongozi wa kundi la kigaidi lenye uhusiano na Saudi Arabia

Waziri wa Intelijinsia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametangaza habari ya kuuawa Abu Hafidh Balush Kinara wa kundi la kigaidi lenye mfungamano na Saudia.

Mahmoud Alavi amesema kuwa vikosi vya intelijinsia na askari usalama wa Iran walio macho wamefelisha njama ya kundi moja la kigaidi lililokusudia kuvuruga usalama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kumuua kiongozi wa ngazi ya juu wa kundi hilo kwa jina la Abu Hafidh Balush anayefahamika kwa utambulisho wa Hosham Azizi. 

Waziri wa Intelijinsia wa Iran amebainisha kuwa harakati za kiusalama za mashirika ya kijasusi zimekuwa zikishuhudiwa katika  mipaka ya Iran na kwamba baadhi ya nyaraka zinaonyesha kuwa mashirika ya kijasusi huwalipa magaidi dola 500,000 kwa kila oparesheni wanayotekeleza, dola 3000 kwa kila mwanachama kwa mwezi na huzilipa famila dola 10,000 kwa kila mwanachama anayeuliwa. 

Mashirika ya ujasusi ya Israel na Marekani, Mossad na CIA ni miongoni mwa waungaji mkono wa magaidi 

Waziri wa Intelijinsia wa Iran ameongeza kuwa mashirika ya kijasusi ya Marekani (CIA), Utawala wa Kizayuni (Mossad), M16 la Uingereza na shirika la ujasusi la Saudi Arabia ni miongoni mwa waungaji mkono wakubwa wa magaidi kwa ajili ya kuvuruga usalama wa Iran. Amesema kuwepo makundi ya kigaidi na kitakfiri katika mipaka ya kusini mashariki na kaskazini magharibi mwa Iran kamwe hakuwezi kuutumbukiza hatarini usalama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.