Magaidi waliotiwa nguvuni Iran wafichua kuhusu misaada wanayopatiwa na Saudia
Mkuu wa Kamisheni ya Bunge ya Usalama wa Taifa na Sera za Nje amesema magaidi waliotiwa nguvuni hapa nchini wametoa taarifa zenye "thamani" kuhusu nafasi ya Saudi Arabia katika kuyasaidia na kuyaunga mkono makundi ya kigaidi.
Akizungumza katika mahojiano na kituo cha habari cha al-Ahdi cha Lebanon, Alaeddin Boroujerdi amesema makundi ya kigaidi yaliyotiwa mbaroni hivi karibuni yametoa taarifa zenye thamani kwa maafisa usalama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu nafasi ya Saudia katika kutoa misaada na uungaji mkono kwa makundi ya kigaidi.
Boroujerdi amefafanua kuwa: "Aal Saud unatumia kila suhula katika eneo na duniani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; na katika suala hili unayasaidia makundi ya kigaidi ili kulilenga taifa la Iran".
Katika miezi iliyopita vikosi vya usalama vya Iran vimepambana mara kadhaa na makundi ya kigaidi katika maeneo ya mpakani na kuzima mipango na njama za makundi hayo. Katika mapigano hayo watuhumiwa wengi wa ugaidi walitiwa mbaroni na kukutwa na mada nyingi za miripuko.
Mwishoni mwa mwezi Juni, Kamanda wa vikosi vya ardhini vya jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) Muhmmad Pakpour alitangaza kuwa baadhi ya magaidi waliotiwa mbaroni nchini wamekiri kuwa Saudia na Marekani zimekuwa zikitoa misaada na kuyaunga mkono makundi yao.
Katika sehemu nyengine ya mahojiano yake na kituo cha habari cha al-Ahdi Alaeddin Boroujerdi amezungumzia pia uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa nchi za Iraq na Syria katika vita dhidi ya ugaidi na kubainisha kwamba leo hii na baada ya miaka mitano muqawama na kusimama imara katika kukabiliana na siasa za Marekani kunashuhudia kupata nguvu zaidi kambi ya muqawama na kusambaratika magaidi likiwemo kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) katika nchi za Iraqa na Syria.../