Rais Rouhani akagua gwaride la heshima Paris, Ufaransa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i145-rais_rouhani_akagua_gwaride_la_heshima_paris_ufaransa
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekagua gwaride la heshima kando ya jengo la kihistoria la Illinois katika mji mkuu wa Ufaransa Paris.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 28, 2016 12:51 UTC
  • Rais Rouhani akagua gwaride la heshima Paris, Ufaransa

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekagua gwaride la heshima kando ya jengo la kihistoria la Illinois katika mji mkuu wa Ufaransa Paris.

Baadaye leo Rais wa Iran anatazamiwa kukaribishwa rasmi na mwenyeji wake Francois Hollande katika Ikulu ya Elysee mjini Paris kwa ajili ya dhifa ya chakula cha jioni, baada ya kukataa kushiriki kwenye karamu ya chakula cha mchana iliyotayarishwa na mwenyeji wake wa Ufaransa, kutokana na ikulu ya Elysée kushikilia msimamo wake wa kuwepo mvinyo katika meza ya chakula iliyotayarishwa kwa heshima ya Rais wa Iran.

Hii ni katika hali ambayo, mapema leo Rais Rouhani amekosoa sera za madola ya kibeberu yanayojipa ukuu, za kutumia njia ya vikwazo dhidi ya nchi zingine kutatua mizozo. Akizungumza katika mkutano uliowaleta pamoja wajasiriamali na wawekezaji wakubwa wa Ufaransa mjini Paris, Rais wa Iran amesema hatua ya kuiwekea Jamhuri ya Kiislamu vikwazo vipya eti kwa sababu ya kuyafanyia majaribio makombora yake ya balestiki ni kinyume cha sheria na kusisitiza kuwa, makubaliano ya nyuklia ya Vienna yanayojulikana kama JCPOA, ni matunda ya kutumiwa mazungumzo na njia za kidiplomasia kutatua migogoro. Rais Hassan Rouhani ameashiria kuhusu uhusiano wa muda mrefu wa Tehran na Paris na kusisitiza kuwa, muda umefika kwa pande mbili hizo kuimarisha zaidi uhusiano wao katika nyuga mbali mbali. Mikataba kadhaa ya kibiashara kati ya Iran na Ufaransa ukiwemo mpango wa nchi hii kununua ndege 114 za shirika la bara Uropa la Airbus, imesainiwa. Kadhalika mashirika ya ndege ya Ufaransa ya Air France na KLM yamesema yako tayari kuruhusu tena safari za ndege zake nchini Iran, baada ya kusimamisha kwa takriban miaka mitano. Safari ya Rais Hassan Rouhani wa Iran nchini Ufaransa ni marhala ya mwisho ya ziara yake barani Ulaya.