Rais Rouhani: Hakuna nchi yoyote inayoweza kuyavuruga makubaliano ya nyuklia
Rais Hassan Rouhani amesema hakuna nchi au rais wa nchi yoyote anayeweza kuyavuruga makubaliano ya nyuklia yaliyosainiwa baina ya Iran na nchi zinaounda kundi la 5+1 pamoja na Umoja wa Mataifa.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya NBC ya nchini Marekani.
Dakta Rouhani amekosoa ukwamishaji unaofanywa na Wizara ya Fedha ya Marekani katika miamala baina ya Iran na mabenki pamoja na asasi nyingine za fedha na kueleza kwamba Iran haina nia yoyote ya kuunda silaha za nyuklia kitakapomalizika kipindi cha miaka minane ya utekelezaji makubaliano ya nyuklia.
Kuhusiana na wakosoaji wa makubaliano ya nyuklia hususan Donald Trump, mgombea urais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Republican ambaye ameyaita kuwa ni 'makubaliano ya kutisha ambayo yumkini yakaishia kwenye Holocaust ya nyuklia', Rais Rouhani ameyatoa maanani madai hayo na kufafanua kwamba makubaliano hayo yamesainiwa na nchi saba pamoja na Umoja wa Mataifa na yanatekelezwa kwa usimamizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).
Katika sehemu nyingine ya mahojiano hayo Rais wa Iran ameashiria ulazima wa kupatikana njia ya ufumbuzi wa kisiasa kwa ajili ya kuhitimisha vita nchini Syria na kusisitiza kwamba vita vya ndani katika nchi hiyo vitaweza kuhitimishwa kwa njia za kisiasa, si kwa vita na mtutu wa bunduki.../