Iran yazima njama za magaidi wakati wa Ashura
(last modified Thu, 13 Oct 2016 07:57:26 GMT )
Oct 13, 2016 07:57 UTC
  • Iran yazima njama za magaidi wakati wa Ashura

Vyombo vya usalama nchini Iran vimetibua njama ya kutekelezwa mashambulizi ya kigaidi hapa nchini wakati wa maombolezo ya Ashura ya kukumbuka tukio chungu la kuuawa Shahidi Imam Hussein AS, mjukuu wa Mtume Mtukufu SAW.

Mahmoud Alavi, Waziri wa Usalama wa Iran amesema maafisa usalama nchini wamezima njama za kutekelezwa mashambulizi ya kigaidi wakati wa marasimu ya Tasua na Ashura, njama zilizokuwa zikipangwa katika mkoa wa kusini wa Fars. Ameongeza kuwa, katika operesheni za kuzima njama hizo, vyombo vya usalama vya Iran vimewatia nguvuni magaidi kadhaa ambao ni raia wa kigeni sambamba na kunasa zaidi ya kilo 100 za mada za miripuko.

Askari wa kikosi maalumu cha kupambana na ugaidi Iran

Aidha Jumanne iliyopita, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran IRGC lilitibua njama nyingine ya kutekelezwa mashambulizi ya kigaidi katika mkoa wa Kordestan, kaskazini magharibi mwa nchi.

Waziri wa Usalama wa Iran amesema kuwa, ushahidi walionao unaonyesha kuwa maadui wa taifa hili wamekuwa wakiwaongoza magaidi hao kutoka nje ya nchi waje kutekeleza hujuma za kigaidi ili kuibua hitilafu za kimadhehebu, njama ambazo zimegonga mwamba kutokana na wananchi wa Iran kuwa macho.

Waislamu wakiadhimisha Ashura Iran

Mwezi Mei mwaka huu, Mahmoud Alavi, Waziri wa Usalama wa Iran alisema vikosi vya usalama nchini vinafuatilia kikamilifu nyendo za maadui wanaopanga kufanya hujuma za kigaidi katika ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu na kwamba maafisa usalama nchini wamefanikiwa kusambaratisha makundi zaidi ya 20 ya kigaidi.